• HABARI MPYA

    Thursday, July 09, 2009

    IRENE UWOYA ALIYEMDATISHA NYOTA WA AMAVUBI























    na mahmoud zubeiry
    KAMA utaanzishwa mjadala wa mabinti wanaotikisa kwenye sanaa ya uchezaji filamu Tanzania, bila shaka yeyote atakayetaja orodha ya wakali hao, jina la mwanadada Irene Pancras Uwoya hataliweka nje ya tano bora.
    Kweli Irene ni miongoni mwa waigizaji bora wa kike wa filamu nchini, ambaye ingawa umaarufu wake ulianzia kwenye fani ya ulimbwende, lakini filamu ndizo zimemstawisha zaidi.
    Irene ana mvuto wa mwonekano, uzuri wa asili na ucheshi unaomfanya daima awe mwigizaji anayevutia kwa yeyote amtazamaye.
    Irene anajua kuigiza katika mazingira yoyote yale, iwe hali ya uchangamfu, majonzi, ‘uchakaramu’ hata umakini wa hali ya juu, yuko tofauti na wasanii wengi wengine nchini wenye vichwa vizito, kiasi cha kuzungumza kama wanasoma, binti huyo ni mweledi. Anavutia anapoonekana akizungumza, akicheka, akifoka, akiwa mwenye furaha, akiwa mwenye huzuni au vyovyote awavyo kwenye filamu alizoigiza.
    Hiyo ni moja kati ya sababu zilizomfanya awe mwigizaji adimu na mwenye thamani kubwa nchini, ambaye watayarishaji na watengenezaji wengi wa filamu nchini wamekuwa wakimbabaikia kwa hilo.
    Kwa Tanzania bado malipo ya wasanii kutokana na kazi zao ni siri, lakini dhahiri kama wapo wanaolipwa vizuri kutokana na sanaa hiyo, Irene ni miongoni mwao, tena katika wale walipwao vizuri mno kutokana na sanaa hiyo nchini.
    Kupanda siku hadi siku kwa hali yake kiuchumi ndicho kielelezo tosha cha binti huyo kupata maslahi mazuri kutokana na sanaa hiyo ya uigizaji ambayo kwa sasa inazidi kupanda chati nchini na kuizidi kete hata fani ya muziki wa Bongo Fleva kwa maslahi.
    Kwa sasa nchini waigizaji bora ndio wanaotamba na magari mazuri, wanajenga nyumba nzuri na wanaishi maisha mazuri pia, hicho ni kielelezo tosha cha mafanikio katika sanaa yao.
    Katika mahojiano maalumu na DIMBA juzi, Irene anasema kwamba anafurahia sanaa hiyo, kwani licha ya kumpanua vizuri kwenye anga la nyota wa Tanzania, pia inampatia maslahi mazuri.
    “Unajua hapa kwetu kila mtu maslahi yake ni siri yake, kwa hivyo hata mimi siwezi kukuambia ninalipwa vipi, ila napenda kukuhakikishia tu kwamba ninalipwa vizuri na ndiyo maana ninafanya filamu nyingi,” anasema mwanadada huyo.
    Irene anasema kwamba matarajio yake ya baadaye ni kuwa mwigizaji wa kimataifa na ndiyo maana mkakati wake mkubwa siku chache zijazo ni kujiendeleza kielimu na kusomea sanaa hiyo.
    Hadi sasa, Irene amekwishacheza filamu tisa, tangu acheze filamu yake ya kwanza, Yolanda miaka mitatu iliyopita, sambamba na akina Mohammed Mwikongi, Ummy Wenceslaus ‘Dokii’, Fadhil Omar ‘Mkono’, Lucy Komba ‘Lorna’, Mrisho Zimbwe ‘Tito’, Dennis Sweya ‘Dino’, Tecla Irenge ‘Nancy’, Pricila Christopher, Eva Clemence na wengineo.
    Filamu nyingine za nyota huyo ni Diversion of Love, Hazard, One Blood, Oprah, Mid Night, Peace of Mind, Tanzanite na Kalunde.
    Baada ya kucheza filamu hizo, Irene sasa anatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa maisha yake, akiwa anatarajiwa kufunga ndoa na mchumba wake, Hamad Ndikumana, raia wa Rwanda, anayecheza soka ya kulipwa nchini Cyprus.
    Anatarajiwa kufunga ndoa Julai 11, mwaka huu, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, mjini Dar es Salaam, baada ya sherehe zote za awali, kufundwa (Kitchen Party) na Kuagwa (Send Off).
    Akizungumzia alivyojiandaa kuyaingia maisha ya ndoa, Irene anasema: “Nimejiandaa vizuri, ninaolewa, nitaheshimu ndoa yangu, nitakuwa mvumilivu ndani ya maisha ya ndoa, nitamsikiliza mume wangu na kufanya yale anayonielekeza na kuacha yale anayonikataza,” anasema.
    Irene anasema kwamba amejifunza mengi kutokana na ndoa za nyota mbalimbali nchini ambazo zilipepesuka na anaamini kikubwa kilichosababisha hayo ni maelewano duni ndani ya nyumba.
    “Ndoa za mastaa (nyota) wengi zinavurugika kwa sababu ya kutoheshimiana ndani ya nyumba, kila mmoja kutaka kuwa juu ya mwenzake, watu hawasikilizani, lakini mimi naahidi kuwa tofauti, siolewi ili niachike, nataka kuingia kwenye maisha ya furaha ndani ya ndoa, lakini katika kila jambo ukimtanguliza Mungu mbele, mafanikio yatakuwapo,” anasema.
    Kuhusu namna atakavyoweza kudumisha maisha ya ndoa na kazi yake ya sanaa, Irene anasema: “Kuolewa haitakuwa sababu ya mimi kuacha sanaa, wala mume wangu kuoa haitakuwa sababu ya yeye kuacha kucheza soka. Tutafanya mambo yetu kwa wakati na ndoa tutaipa nafasi yake.
    “Mume wangu anacheza mpira Cyprus, kama Mungu akimjaalia kupata timu nyingine nchi nyingine, tutahamia huko. Lakini mimi wakati wowote nitapanda ndege kwenda sehemu yoyote nitakapopata dili ya kwenda kutengeneza filamu, haitaleta matatizo kwetu, kwa sababu tumekwishakubaliana,” anasema.
    Siku za nyuma baadhi ya magazeti ya udaku yamekuwa yakiandika habari ‘chafu’ kuhusu binti huyo, je, hii anaichukuliaje? “Hainipi tabu, kwa sababu yote yanayoandikwa ni uongo, ninaingia kwenye ndoa yangu nikiwa huru kifikra na mawazo, nayapuuza yote ya uzushi yaliyotokea na yatakayotokea,” anasema Irene, ambaye kwenye tuzo za filamu mwaka jana, aliibuka na ya Mwigizaji Bora Msaidizi.
    Irene alizaliwa Desemba 18 mwaka 1988 mjini Dodoma, kabla ya kuanza elimu yake ya msingi katika shule ya Mlimwa hadi darasa la tano na kuhamia Bunge ya Dar es Salaam alikomalizia elimu yake hiyo. Sekondari alisoma mjini Kampala, Uganda katika shule iitwayo Greenville, alikohitimu Kidato cha Nne.
    Aliporejea nchini, Irene alijitosa kwenye fani ya ulimbwende na alianza kushiriki shindano la Miss Chang’ombe ambako aliibuka mshindi wa kwanza mwaka 2006, hivyo kupata tiketi ya kushiriki Miss Temeke, ambako alikuwa mshindi wa pili. Irene alipata tiketi ya kushiriki Miss Tanzania mwaka huo ambako alikwenda kushika nafasi ya tano, hivyo kuingia kwenye orodha ya warembo bora waliowahi kushiriki shindano hilo la taifa. Kutoka hapo, bi harusi huyo mtarajiwa, amekuwa mwigizaji nyota wa filamu Tanzania, akila sahani moja na wakali kama Ray, Kanumba, Hawa Mkamba na wengineo.

    HAMAD NDIKUMANA NI NANI?
    Hamad Ndikumana Ismael aliyezaliwa Oktoba 5, mwaka 1978 mjini Kigali, Rwanda, ambaye mbele ya mashabiki wa nchini mwake anajulikana kama Kataut, ni beki wa kimataifa wa Amavubi, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Daraja la Kwanza
    A. E. Lemesos ya Cyprus, aliyojiunga nayo akitokea AC Omonia ya nchini humo pia.
    Awali alichezea Anorthosis, KV Mechelen, APOP Kinyras Peyias, Nea Salamina na KAA Gent. Aliiwezesha Rwanda kupata nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2004 nchini Tunisia, ingawa tangu Amavubi ifungwe nyumbani na Angola 1-0 katika mechi ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, hajaitwa tena timu yake ya taifa. Hiyo ilitokana na kutuhumiwa kuwasaidia Angola kushinda mchezo huo muhimu, ambao uliwapa tiketi ya kucheza fainali za kwanza za Kombe la Dunia. Amejiunga na AEL Limassol Julai mwaka jana, akisaini mkataba wa miaka mitatu. Beki huyo aliibukia kwenye klabu ya Rayon Sport ya Rwanda msimu wa 1998-1999 na alikuwamo kwenye kikosi cha klabu hiyo kilichotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, visiwani Zanzibar chini ya kocha Raoul Jean Pierre Shungu, aliyewahi pia kuinoa Yanga ya Dar es Salaam.
    Kwa kufunga ndoa na Irene kanisani, ina maana Ndikumana anaachana na dini yake ya Kiislamu sasa kwa ajili ya mlimbwende huyo wa Kitanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    1 comments:

    edy said... April 6, 2010 at 1:12 PM

    huyu dada ameumbika ucpime

    Item Reviewed: IRENE UWOYA ALIYEMDATISHA NYOTA WA AMAVUBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top