• HABARI MPYA

    Friday, April 20, 2012

    MKUTANO MKUU TFF UMEKAA KISANII MNO

    Rais wa TFF, Leodegar Tenga
    MKUTANO Mkuu wa mwaka wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unafanyika kesho kwa siku mbili, hadi Jumapili kwenye ukumbi wa NSSF Water Front mjini Dar es Salaam.
    Wajumbe wa mkutano huo walianza kuwasili leo na kufikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom.
    Mkutano huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda 11, miongoni mwao ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011, bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited accounts).
    bongostaz.blogspot.com tunaamini Mkutano huo ndio umebeba dira ya soka yetu siku zijazo, iwapo hoja za msingi zitajadiliwa kwa uwazi na mapana marefu na hatua zitachukuliwa kwa manufaa ya soka yetu.
    Tunasikitika tu, ajenda ni nyingi na bado kuna mambo ambayo hayajaingizwa kwenye ajenda, lakini yanapaswa kujadiliwa na kupatiwa majibu, ila muda ni mchache.
    Kesho jioni kuna mechi kati ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes dhidi ya Sudan, maana yake kwa kesho Mkutano hautadumu zaidi ya saa nne.
    Ratiba inasema Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, lakini kulingana na desturi zetu za Kitanzania unaweza ukaanza hata saa tano.
    Baada ya hotuba ndefu za Mheshimiwa Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Rais wa TFF- Leodegar Tenga kuna ajenda hata moja itaweza kujadiliwa kwa kina kweli kabla ya watu kuinuka kwenda Uwanja wa Taifa?
    Kana kwamba hiyo haitoshi, Jumapili ni siku ambayo Wajumbe wengi wataamkia kwenye ibada kanisani, wengine watakuwa na uchovu wa starehe za wikiendi na kadhalika.
    bongostaz.blogspot.com inachukulia huu kama ni mzaha katika mambo ya msingi kuhusu mustakabali wa soka letu na kwa sababu hiyo, TFF ijue kwa mara nyingine inajitia doa.
    Soka ya Tanzania imeporomoka, mambo mengi yanaenda ovyo- haijulikani Kombe la Taifa litafanyika mwaka huu au la baada ya kuwapo taarifa kwamba waliokuwa wadhamini wa michuano hiyo, Kilimanjaro Beer sasa wanakuwa wadhamini wa Taifa Stars.   
    Hiyo haipo ndani ya ajenda za Mkutano Mkuu, lakini watu watapenda kujua.
    Taarifa kwamba hati ya Uwanja wa Karume imewekwa bondi katika benki moja nchini kutokana na deni kubwa linaloikabili TFF- hii pia watu wanapenda kujua.
    Mustakabli wa benchi la ufundi la timu ya taifa- mfumo wa uendeshwaji wa Ligi Kuu na kadhalika watu watapenda kusikia vilijadiliwa katika Mkutano Mkuu, lakini katika mazingira ya muda huwezi kuona nafasi pana.
    bongostaz.blogspot.com kwa kiasi kubwa inasikitishwa na namna ambavyo Mkutano Mkuu umepangwa- uko kisanii mno. Uko kwa ajili ya kutimiza tu utaratibu kama Katiba inavyoagiza na si Mkutano wenye lengo la kutafuta tija.
    Mwisho wa siku hatuna cha kufanya zaidi ya kuwaachia wenye dhamana, wakubwa waendelee kutuburuza na kuzidi kuichimbia kaburi soka ya nchi hii.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUTANO MKUU TFF UMEKAA KISANII MNO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top