• HABARI MPYA

    Wednesday, April 04, 2012

    WACHEZAJI YANGA WAPUNGUZIWA ADHABU, POINTI ZA COASTAL MMH!

    Kikosi cha Yanga
    KIKAO cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kimemalizika majira ya saa 5:30 usiku huu na kimegoma kujadili suala la klabu ya Yanga kuponywa pointi na Kamati ya Ligi Kuu ya Vodacom ya Tanzania Bara, ikiitaka klabu hiyo ikate rufaa maaulm juu ya hilo.
    Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga aliyekuwapo kwenye kikao hicho, ameiambia bongostaz dakika chache zilizopita kwamba, kwa kuwa hawakuwasilisha rufaa ya kupinga kupokonywa pointi za Coastal Union, wametakiwa kufanya hivyo ndipo suala hilo lijadiliwe.
    Hata hivyo, Nchunga alisema kwamba Kamati hiyo, imewapunzia adhabu wachezaji wote watano wa Yanga walioadhibiwa na Kamati ya Ligi Kuu katika kikao chake cha Machi 12, mwaka huu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu walioufanya kwenye mechi ya Azam FC, Machi 10, mwaka huu, Uwanja wa Taifa.
    Hao ni Stefano Mwasyika aliyempiga ngumi refa wa mechi hiyo Israel Nkongo ambaye awali alihukumiwa mwaka mmoja na faini ya Sh Milioni 1, ambaye sasa amehukumiwa kukosa mechi zilizobaki za msimu na faini ya Sh. Milioni 2 sawa na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye awali alihukumiwa kukosa mechi tatu na adhabu ya Sh, 500,000.
    Beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye awali alihukumiwa kukosa mechi sita na faini ya Sh. 500,000, sasa atakosa mechi tatu na faini ya tatu, wakati viungo Nurdin Bakari na Omega Seme sasa watakosa mechi mbili na faini ya Sh. Milioni 1 kila mmoja.
    Awali, Nurdin alihukumiwa mechi tatu na faini Sh. 500,000 sawa na Omega Seme.
    Yanga ilipokonywa pointi hizo kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika mechi dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga Jumamosi,
    Coastal ilicheza chini ya pingamizi katika mchezo huo, ambao ilifungwa 1-0 ikipinga klabu hiyo kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ikidai alikuwa hajamaliza adhabu yake ya kukosa mechi tatu baada ya kupewa kadi nyekundu kwa vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam FC
    Nchunga alisema waliamua kumtumia Cannavaro baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, Alfred Tibaigana kusitisha adhabu zote zilizotolewa na Kamati ya Ligi kuwafungia wachezaji watano wa Yanga kwa kufanya fujo kwenye mechi na Azam FC, ikiwemo kumpiga refa.
    Awali, wiki iliyopita Tibaigana alisitisha adhabu zote akidai kwamba Kamati ya Ligi haina mamlaka ya kutoa adhabu, ispokuwa Kamati yake.
    Kwa matokeo hayo, Yanga sasa inabaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 44, baada ya kucheza mechi 21, wakati Azam iliyocheza mechi 22 ina pointi 46 na inaendelea kubaki nafasi ya pili.
    Simba inayoongoza ligi hiyo kwa pointi zake 50, nayo imecheza mechi 22, moja zaidi, dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga.
    Nchunga alisema mapema kesho watawasilisha rufaa nyingine kwa Kamati hiyo, kupinga maamuzi ya Kamati ya Ligi Kuu kuwapokonya pointi za ushindi wa Tanga kwa sababu walimtumia beki huyo baada ya maamuzi ya Kamati ya Tibaigana.
    Aidha, Nchunga alikana taarifa za kwamba walionywa kutomchezesha Cannavaro katika mechi ya Tanga kabla ya mchezo huo.
    “Sikusikia kitu kama hicho, kwa nini tumtumie kama tungepewa angalizo, tumecheza mechi ngapi bila Cannavaro na tumeshinda, iweje tulazimishe kumtumia kwenye mechi hiyo,”alisema Nchunga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WAPUNGUZIWA ADHABU, POINTI ZA COASTAL MMH! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top