• HABARI MPYA

    Tuesday, May 22, 2012

    BREAKING NEWS: NURDIN ACHANIKA PAJA, KUWAKOSA MALAWI, ULI, SAMA GOAL WATUA KAMBINI



    Nurdin 'Tshabalala' Bakari'
    WAKATI washambuliaji wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wamewasili kwenye kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana usiku, habari mbaya ni kwamba kiungo Nurdin Bakari Hamadi wa Yanga ameumia nyama za paja na anatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki moja kuanzia leo.
    Meneja wa timu ya taifa, Taifa Stars, Leopold Mukebezi ‘Taso’ ameiambia BIN ZUBEIRY dakika kadhaa zilizopita kwamba, Nurdin aliumia jana katika mazoezi ya jioni na baada ya uchunguzi wa daktari leo, imebainika anatakiwa apumzike kwa siku saba.
    “Kwetu ni pigo, kwa sababu huyo mchezaji aliitwa na mwalimu na alikuwa kwenye mipango ya timu. Ila hakuna jinsi, tutalazimika kuendelea na hawa tulionao,”alisema beki huyo wa kikosi cha Stars kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Kwa ujumla, Taso alisema maendeleo ya kambi, iliyopo Tansoma Hotel, Dar es Salaam ni mazuri na Kocha Mkuu Mdenmark, Kim Polusen anaendelea vizuri na wasaidizi wake, Sylvester Marsh na Juma Pondamali kuwanoa vijana.
    Taso amefurahishwa na nidhamu ya wachezaji na kujituma kwao mazoezini na anasema hiyo inatia moyo kuelekea mchezo wa Jumamosi na Malawi, ambao ni wa kirafiki kabla ya kumenyana na Ivory Coast kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
    Stars inadhaminiwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro, ambao pia ni wadhamini wa klabu kongwe Tanzania, Simba na Yanga.
    Wakati huo huo: Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah Malabeja amesema kwamba Malawi inatarajiwa kuwasili keshokutwa nchini, ikiwa na msafara wa watu 27.

    Baadaye Malawi itakwenda Zanzibar kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes itakayofanyika Mei 28 mwaka huu kabla ya kuondoka Mei 30 mwaka huu kwenda Uganda ambapo Juni 2 mwaka huu itcheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BREAKING NEWS: NURDIN ACHANIKA PAJA, KUWAKOSA MALAWI, ULI, SAMA GOAL WATUA KAMBINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top