• HABARI MPYA

    Sunday, May 20, 2012

    MALAWI KUMCHAGUA FIRST ELEVEN POULSEN STARS

    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen (pichani kushoto) amesema atautumia mchezo wa kirafiki wa Kimataifa kati ya timu yake na Malawi uliopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi ijayo kupata kikosi cha kwanza cha timu hiyo. 
    Gazeti la serikali, Habari Leo la leo limeandika; Kim kama ambavyo anapenda kuitwa ili kumtofautisha na kocha aliyemtangulia Jan Poulsen alisema hayo baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jana asubuhi kuwa atautathmini uwezo wa wachezaji wa timu hiyo kwenye mechi na kupata kikosi kitakachoivaa timu ya Taifa ya Ivory Coast Juni 2 Abijan. 
    Taifa Stars imeweka kambi yake kwenye Hoteli ya Tansoma iliyopo Kariakoo jijini Dar es 
    Salaam ikijiandaa na mchezo wa awali wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil 2014 dhidi ya Ivory Coast ambayo ni miongoni mwa miamba ya soka ya Afrika lakini Kim haonekani kuingiwa hofu na mechi hiyo. 
    “Ndio nafahamu Ivory Coast ni timu kubwa inayoundwa na wachezaji wazoefu, hiyo ni changamoto kwangu na nafurahia kucheza na timu za namna hiyo,”alisema Kim. 
    Akizungumzia falsafa yake ya ufundishaji Kim tofauti na makocha wengi wanaopenda mfumo 
    wa soka la kujihami hasa wanapoanzia ugenini alisema falsafa yake ni kucheza soka la kushambulia na kuhakikisha washambuliaji wa timu wanatumia vyema kila nafasi watakayoipata. 
    “Nitashambulia nikiwa Abijan na nitataka wachezaji wangu kutumia kila nafasi itakayopatikana kwenye mchezo huo, lakini pia lazima tujilinde vizuri ili tusifungwe,” alisema Kim. 
    Ingawa alisema kuwa kwa sasa anauwazia mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi Jumamosi ijayo kwani ndio utakaompa picha ni kwa kiwango gani wachezaji wa timu hiyo wamepokea 
    mafundisho yake. 
    Alisifu ushirikiano unaoneshwa na wachezaji wazoefu wa timu hiyo kuwasaidia wachezaji 
    chipukizi katika kushika na kuelewa mafundisho yake. 
    Wachezaji wote wamejiunga na kambi ya timu hiyo isipokuwa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, ambao alisema wanamalizia mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na watawasili nchini kesho kuungana na wenzao. 
    Mbali na washambuliaji hao pia alikosekana kiungo mchezeshaji wa Simba Haruna Moshi 
    ambaye yuko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alikosindikiza msiba wa kiungo wa Simba 
    Patrick Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari Alhamisi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALAWI KUMCHAGUA FIRST ELEVEN POULSEN STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top