• HABARI MPYA

    Thursday, July 05, 2012

    OKWI AWAKANA YANGA, ASEMA AKIKOSA TIMU ITALI, ANARUDI SIMBA


    Kaburu akiwaonyesha Waandishi mkataba wa Okwi na Simba 


    Mkataba wa Okwi na Simba

    Soma vipengele hapo

    Kaburu akizungumza na Waandishi wa Habari

    Kaburu akiwasikiliza sauti ya Okwi waandishi

    Hapa anafunguka kwa hisia kali
    Na Prince Akbar
    WAKATI Mshambuliaji Emmanuel Okwi amekanusha kusaini Yanga, uongozi wa klabu yake, Simba umesikitishwa na habari zilizovumishwa kwenye vyombo vya habari kuhusu mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda kujiunga na wapinzani wa jadi, Yanga SC.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo, makamo makuu ya klabu Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, alisema kwamba habari hizo hazina ukweli wowote, ni kinyume cha maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na zina lengo la kupotosha ukweli na kuwanyima raha wale wote wenye mapenzi mema na Simba.
    “Gazeti kama la Spoti STAREHE limekwenda mbali zaidi kwa hatua yake ya kutaka kuufitinisha uongozi na wapenzi na wanachama wake kwa kudai kuwa uongozi unafikiria tu kumuuza Okwi bila ya kuangalia mkataba wake.
    Kwa mujibu wa gazeti hilo, mkataba wa Okwi umemalizika leo na ndiyo maana ameamua kusaini Yanga akiwa mchezaji huru,”alisema Kaburu na kuongeza;.
    “Ukweli ulivyo. Emmanuel Okwi alisaini mkataba mpya wa kuichezea Simba mnamo mwaka jana na mkataba huo unamfanya kuwa mchezaji halali wa klabu yetu hadi mwaka 2013. Baada ya mkutano huu, nitawaonyesha waandishi nakala ya mkataba wa Okwi na Simba. Hivyo taarifa kwamba mchezaji huyo hana mkataba na Simba ni za uongo, uongo mtupu,”alisema.
    “Hivi ninavyozungumza nanyi, Okwi yuko kwao nchini Uganda akishughulikia viza ya kwenda nchini Italia ambako anatarajiwa kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika moja ya vilabu vya Ligi Kuu ya Italia (Serie A),”alisema Kaburu.
    Okwi
    Kaburu alisema kwamba Okwi ni miongoni mwa wachezaji wenye uelewa wa hali ya juu wa haki na wajibu wao na hawezi kufanya mambo kama ambavyo yameripotiwa katika vyombo vya habari na kusambazwa kwa njia ya sms siku nzima ya jana.
    Aidha, alisema uongozi wa Simba SC unavitaka vyombo vya habari vilivyoripoti kuhusu Okwi kuhamia Yanga (gazeti la Bingwa na lile la Spoti STAREHE) kuomba radhi katika kipindi cha siku saba kuanzia leo la sivyo uongozi utachukua hatua kali za kisheria dhidi yao.
    “Tayari tumewasiliana na mwanasheria wa klabu ambaye ameelekeza kwamba ni lazima vyombo hivyo viombe radhi na viuambie umma kwamba vilisema uongo na vinajutia kosa hilo la kimaadili na habari hiyo itoke katika ukurasa wa mbele katika namna ileile ambayo habari ya leo ilitoka.
    Pia, uongozi wa Simba unaviomba vyombo vya dola vichunguze ni nani anahusika na usambazwaji wa taarifa hizi kwenye simu na vyombo vya habari kwani zina hatari ya kuchafua hali ya amani na utulivu nchini,”alisema.
    Aidha, Kaburu alimpigia simu Okwi na kuzungumza naye huku akiwasikilizisha Waandishi wa Habari. Katika mazungumzo hayo, alisema hana mpango wa kusaini Yanga na kwa sasa yuko kwao Uganda akifuatilia visa ya kwenda Italia ndani ya siku mbili hizi, ambako anatakiwa na klabu ya Parma ya Serie A.
    “Akili yangu kwa sasa ni kucheza Ulaya, na hata kama nitakosa nafasi Italia, basi kama ni kurudi Tanzania, basi nitaendelea kucheza Simba siyo Yanga,”alisema Okwi katika mazungumzo yake na Kaburu kwa simu kutoka Uganda.
    Mbali na Parma, Okwi pia anatakiwa na Etoile du Sahel ya Tunisia, Mamelodi Sundown na Orlando Pirates za Afrika Kusini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI AWAKANA YANGA, ASEMA AKIKOSA TIMU ITALI, ANARUDI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top