• HABARI MPYA

    Saturday, September 01, 2012

    SIMBA WAPAMBANA NA PINGAMIZI LA REDONDO, WATAKA MILIONI 80 WAONDOE PINGAMIZI LA YONDAN YANGA

    Redondo

    Na Prince Akbar
    JITHADA za chini zinaendelea kwa viongozi wa Simba SC, kuhakikisha wanamalizana na klabu ya Azam FC juu ya kiungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’, aweze kuichezea klabu hiyo katika Ligi Kuu.
    Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani na ili kumuachia kiungo huyo iliyemsajili kutoka Simba miaka mitatu iliyopoita, inataka dola za Kimarekani 50,000 ingawa Simba wamefika dola 20,000 ambazo pia wameomba kulipa kwa awamu.
    Habari zaidi zinasema kwamba, Simba nayo inataka dola 60,000, zaidi ya Sh. Milioni 80 kutoka kwa Yanga, ili wawauzie beki Kevin Yondan. Simba imepinga Yondan kusajiliwa Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
    Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine 2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu hiyo.
    Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
    Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
    Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
    Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
    Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
    Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
    Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAPAMBANA NA PINGAMIZI LA REDONDO, WATAKA MILIONI 80 WAONDOE PINGAMIZI LA YONDAN YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top