Kikosi cha Tanznaia cha Airtel Rising Star kilichotoa sare jana |
Na Princess Asia
TIMU ya taifa ya Tanzania ya Airtel Rising Stars jana
imetoka sare ya bao 1-1 na Burkina Fasso, katika michuano ya Airtel Rising Star
Afrika, Uwanja wa Nyayo, mjini Nairobi, Kenya.
Matokeo hayo yanaiweka Tanzania shakani kusonga
mbele katika michuano hiyo baada ya jana kuianza vibaya kwa kukubali kufungwa
bao 1-0 na Gabon katika mchezo wake wa kwanza.
Kufuatia matokeo hayo Tanzania inasubiri bahati tu
ili kusonga mbele kwani sasa itabidi kushinda mchezo wake wa mwisho
utakaofanyika kesho 23/08/2012 dhidi ya Zambia na wakati huo huo kuiombea Gabon
iifungwe na Zambia katika mchezo wao wa mwisho. Kila kundi itatoa timu moja kusonga
mbele hatua ya robo fainali zinazotarajiwa kuanza kesho kutwa.
Katika mchezo wa jana, Burkina Fasso ndiyo ilikuwa
ya kwanza kupata bao la kushtukiza katika dakika ya kwanza ya kipindi cha pili
na hivyo kuwafanya vijana hao wa Tanzania kutulia na kuanza kucheza pasi za kuonana
hali iliyozaa matunda dakika kumi baadaye.
Goli la kusawazisha la Tanzania lilipachikwa kimiani
na mshambuliaji wake hatari Paulo Balama aliyepokea pasi akiwa kati ya uwanja
na kuchanja mbuga kuelekea langoni mwa wapinzani wao, ambapo kabla ya kufunga
aliwapunguza mabeki watatu na kisha kumlamba chenga kipa wa Burkina Fasso na
kuachia kiki kali iliyokwenda moja kwa moja wavuni.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Kocha na mkuu
wa msafara wa timu
ya Tanzania, Salum Madadi alisema vijana wake
walicheza vizuri isipokuwa tatizo ni kutopata muda wa kutosha wa wachezaji wake
kuzoeana hasa ikizingatiwa kuwa timu hiyo inaundwa na kombaini ya wachezaji
kutoka mikoa sita tofauti.
"Kwa mfano mchezo wetu wa juzi dhidi ya Gabon
vijana walicheza vizuri sana pamoja na tatizo la kutozoeana hata hivyo waliweza
kuwabana wapinzani kwa muda mwingi na hata kufika langoni mwa wapinzani wetu kwa
kupiga mashuti kadhaa ila bahati haikua yetu tu," alisema Madadi.
Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa jana kwa
wanaume ni Kenya kutoka sare ya 1-1 na Ghana, Malawi pia kutoka sare ya 1-1 na
Madagascar, Nigeria kutoka sare ya 1-1 na Niger, Congo DRC kuichakaza Chad bao
5-0 na Zambia kuichapa Burkina Fasso 5-0. Kwa upande wa wanawake Congo DRC iliichakaza
Burkina Fasso magoli 8-0, Ghana nayo ikaichapa Kenya bao 7-2, Chad ikaifunga
Nigeria bao 1-0 na Uganda kuifunga Sierre Leone
3-0.
Michuano hiyo ya Airtel Rising Stars kwa ngazi ya
Afrika iliyoanzishwa kwa lengo la kuibua vipaji kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 17, Inafikia kilele keshokutwa kwa bingwa kupatikana ambapo mshindi huyo atapata
nafasi kwa wachezaji wa timu nzima kuhudhuria kliniki ya soka ya kimataifa
itakayoendeshwa na jopo la makocha kutoka klabu ya Manchester United na Arsenal
za Uingereza itakayofanyika kuanzia Agosti 26 hadi 30 mwaka huu jijini Nairobi.
0 comments:
Post a Comment