![]() |
Viongozi wa Yanga, kushoto Mussa Katabaro na Seif Ahmad 'Magari' wakiwa taaban Uwanja wa Jamhuri jana |
Na Mahmoud Zubeiry,
Morogoro
KIPIGO cha
mabao 3-0 ambacho Yanga imechapwa na wenyeji Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa jana, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, kimemkasirisha Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji
amefoka mno.
Chanzo chetu
cha habari kutoka Yanga leo, kimesema kwamba Manji alipiga simu kuulizia
matokeo na kufoka sana baada ya kuambiwa timu imefungwa mabao 3-0. “Manji
amekasirika sana, alipiga simu, alipoambiwa timu imefungwa akafoka
sana,”kilisema chanzo chetu kutoka Yanga jana.
Viongozi wa
Yanga walioambatana na timu hapa mjini hapa, akiwemo Seif Ahmad ‘Magari’ na
Mussa Katabaro walisikitishwa na hali hiyo na hawakuwa tayari kusema chochote.
Manji akizungumza na wachezaji baada ya kutwaa Kombe la Kagame. |
Lakini
habari za ndani zinasema hali hiyo imeanza kuwashangaza hata makocha na
wachezaji, kwa sababu timu yao ilikuwa vizuri na ghafla inaanza kubadilika.
Yanga
itarejea Dar es Salaam leo kuanza maandalizi ya mchezo wao ujao, dhidi ya JKT
Ruvu Jumamosi, lakini kabla ya hapo kutakuwa na kikao kikali juu ya mwenedo wa
timu katika mechi mbili za mwanzo.
Katika
mchezo wa kwanza ambao Yanga ililazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons
mjini Mbeya, kocha Mbelgiji wa klabu hiyo alilalamikia malazi mabovu katika
hoteli waliyofikishiwa, lakini jana alisema malazi yalikuwa mazuri na wachezaji
walikuwa vizuri kabla ya mechi.
Labda ni
Uwanja mbovu, hiyo ni sababu iliyobakia, lakini mechi ijayo Yanga itacheza
kwenye Uwanja mzuri wa Taifa, Dar es Salaam waliouzoea dhidi ya JKT ambayo jana
ilipigwa 2-0 na Simba pungufu.
Mambo mawili
yanatazamwa kwa sasa, moja mfumo wa kucheza kwa kujihami zaidi na pili
kujiamini kupita kiasi, labda yanaweza kuwa yanachangia matokeo mabaya.
Wachezaji wa Yanga kwa sasa wanaonekana ‘kujisikia’ mno baada ya matokeo mazuri
ya awali, ikiwemo kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame na hawachezi kwa kujituma kama mwanzo.
Kuhusu
mfumo, hakuna kilichobadilika sana Yanga, bado ni ule ule wa kutumia mabeki
watupu wingi ya kushoto, ambao uliwapa Kombe la Kagame, labda tatizo la
‘kujisikia’ kwa wachezaji na kudharau timu pinzani linaweza kuwa la msingi
katika suala hili.
Katika
mchezo wa jana, Yanga ilizidiwa mno na hadi mapumziko, tayari Mtibwa Sugar
walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na beki wa kati, Dickson Daudi
dakika ya 11 akiunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto Malika Ndeule.
Bao hilo
lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambao walishindwa kumuweka ulinzi
mchezaji mrefu kuliko wote, Daudi.
Yanga
walijaribu kutaka kusawazisha, lakini mipango yao haikuwa na tija na kujikuta
wakiendelea kushambuliwa na dakika ya 43, Hussein Javu aliwainua tena vitini
mashabiki wa Simba waliokuwa wakiwashangilia kwa nguvu leo kwa kufunga bao la
pili.
Kwa ujumla
kipindi cha kwanza, Yanga walicheza ovyo- pasi zao nyingi zilikuwa hazifiki,
walishindwa kuwabana wapinzani wao na zaidi Haruna Niyonzima alishindwa
kuiongoza vema timu, jambo ambalo lilifamnya kiungo mkabaji Athumani Iddi
‘Chuji’ kupanda mbele zaidi kusaidia, ingawa haikusaidia.
Mabeki
wawili wa kati wa Mtibwa, Daudi na Salvatory Ntebe waliwadhibiti vema
washambuliaji wawili wa Yanga, Hamisi Kiiza na Saidi Bahamnuzi katika dakika 45
za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha
pili, Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet alianza kwa mabadiliko akiwatoa Frank
Damayo na David Luhende na kuwaingiza Simon Msuva na Stefano na Mwasyika,
lakini bado ukuta wa Mtibwa ulikuwa mgumu mbele ya Watoto wa Jangwani.
Katika
kuongeza mashambulizi, Mtakatifu Tom alimtoa beki Mbuyu Twite na kumuingiza na
mshambuliaji Didier Kavumbangu, lakini bado mambo yaliendelea kuwa magumu kwa
Yanga.
Dakika ya 86
Hussein Javu aliifungia Mtibwa bao la tatu kwa shuti la mbali, wakitoka
kushambuliwa na kufikia hapo, Yanga ‘walikufa’ na mashabiki wao wakaanza
kuuacha Uwanja wa Jamhuri.
Huu unakuwa
mchezo wa pili kwa Yanga tangu kuanza kwa ligi wakiwasononesha mashabiki wao,
baada ya mechi ya kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons kwenye
Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Waswahili
wanasema siku ya kufa nyani, miti yote huteleza, Hamisi Kiiza alipaisha mkwaju
wa penalti dakika ya 89, baada ya Daudi kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Yanga SC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul,
, Mbuyu Twite/Kavumbangu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi
‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi
Kiiza na David Luhende/Stefano Mwasyika.
Mtibwa Sugar; Shaaban Hassan Kado, Malika Ndeule, Issa
R Issa, Dickson Daudi, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate/Babu Ally
Seif, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Vincent Barnabas/Ally
Mohamed ‘Gaucho’.
Katika mechi
nyingine, Simba SC imeendeleza wimbi la
ushindi, baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
licha ya kucheza pungufu baada ya Emanuel Okwi kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Mabao ya Simba yalitiwa kimiani na
viungo Amri Kiemba na Haruna Moshi ‘Boban’ na kwa matokeo hayo, Simba
inaendelea kuongoza ligi kwa kufikisha pointi sita, baada ya awali kuifunga
African Lyon 3-0.
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’,
Amir Maftah, Shomary Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna
Moshi ‘Boban’, Daniel Akuffo, Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo,
Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Azam imelazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji
Toto African, Uwanja wa Kaitaba Bukoba, wenyeji Kagera Sugar wametoka sare
ya bila kufunga na JKT Oljoro ya Arusha, wakati Uwanja wa Sokoine Mbeya,
wenyeji Prisons wametoka sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga na kwenye Uwanja
wa Chamazi, African Lyon imeifunga Polisi Morogoro 1-0, wakati Uwanja wa
Mabatini, Mlandizi, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Mgambo JKT.
0 comments:
Post a Comment