• HABARI MPYA

    Friday, October 12, 2012

    AZIM DEWJI AWAPA MANENO YA HEKIMA NA MAANA SIMBA, YANGA ILI ZIJITAMBUE

    Azim Dewji

    Na Prince Akbar
    WAKATI klabu za Yanga na African Lyon zikiendelea kusuguana na mdhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya simu ya mkononi ya Vodacom, klabu za soka nchini zimeaswa kuanza kujitambua ili ziweze kunufaika kwa mambo mengi zaidi, badala ya kutumia muda mrefu kulumbana kwa mambo madogo, akitolea mfano wa nembo ya Vodacom katika
    jezi za klabu.
    Ushauri huo umetolewa na mfadhili wa zamani wa Simba, mfanyabiashara Azim Dewji aliyesema kuwa, kama klabu za Tanzania zingekuwa zinajitambua, kamwe zisingepoteza muda kwa malumbano ya nembo, bali maslahi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, alisema klabu kubwa kama Simba na Yanga, zinapaswa kujenga hoja nzito kwa wadhamini, ilin ziweze kunufaika zaidi kwa kuwa zina thamani kubwa kutokana na ukongwe wake na utajiri wa wafuasi kote ndani na nje ya Tanzania.
    “Sawa wana haki, lakini klabu zetu ifike mahali zijitambue.
    Wavuke hapo, mfano Simba na Yanga si zijenge hoja za kupata fedha zaidi kwa wadhamini kwamba ili zivae jezi na nembo, zilipwe vizuri kulingana na hadhi halisi ya klabu hizi.
    “Haiingii akilini kuona zimeshindwa kujenga ushawishi hata baada ya kuwekwa kundi moja na timu ambazo hazina wanachama wala ofisi, lakini kwa mujibu wa mkataba zote zinalipwa sh milioni 7 kwa mwezi.
    “Jamani, hivi Yanga yenye utitiri wa wanachama na wafuasi, utajiri wa majengo mfano jingo lake lina thamani ya bilioni 2, inalipwaje sawa na African Lyon ambayo haina wanachama wala ofisi? “Si kama naidharau Lyon, la hasha, bali ndio uhalisia kwa sababu kama
    ni kunufaika, Vodacom itanufaika zaidi kwa Yanga kutokana na wafuasi wake wengi kuliko Lyon, kwanini wasitumie mwanya huo kujenga hoja?”
    alihoji Dewji na kuongeza kuwa, hadhi ya klabu za Simba na Yanga ni angalau kila moja iambulie sh milioni 250 kwa mwaka, na jezi za hadhi ya juu kulingana na hadhi ya klabu zenyewe.
    Aidha, alisema udhamini mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ni uthibitisho tosha kuwa thamani ya Simba na Yanga. TBL kupitia bia ya Kilimanjaro, inazidhamini Simba na Yanga kila moja kwa wastani wa sh bilioni 1.5 kwa mwaka, udhamini ukigusa mishahara ya wachezaji na benchi la ufundi, mabasi, vifaa vya michezo, gharama za mikutano ya
    kila mwaka na kadhalika.
    “Una sasa, TBL si wadhamini wakuu wa soka ya nchi hii, lakini klabu hizi zinanufaika, kama ukweli ndio huo kwa nini wasimbane mdhamini wa ligi ili wanufaike zaidi na badala yake wanabaki na malumbano ya nembo pekee? Ni wakati wa klabu zetu kubadilika kwa sababu kote ulimwenguni, soka ni biashara kubwa mno,” alisema.
    Kauli ya Dewji imekuja huku klabu za Yanga na Lyon zikiwa katika mgogoro juu ya kutovaa jezi zenye nembo ya Vodacom, Yanga ikisema haiko tayari kuvaa jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini huku Lyon ikitaka iruhusiwe kuvaa jezi za mdhamini wake binafsi, kampuni nyingine ya simu za mkononi ya Zantel.
    Kutokana na mvutano huo, klabu hizo zimejiingiza katika hatari ya kuadhibiwa, kwani Shirikisho la Soka nchini (TFF) limetishia kuchukua hatua dhidi ya klabu zinazokwenda kinyume na matakwa ya mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu ambao hata hivyo klabu zinalalamikia kuwa hauko wazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZIM DEWJI AWAPA MANENO YA HEKIMA NA MAANA SIMBA, YANGA ILI ZIJITAMBUE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top