• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2012

    BEKI LA KAGERA LAZIMWAGA MATE SIMBA NA YANGA

    Benjamin Effe akumdhibiti Mrisho Ngassa

    Na Mahmoud Zubeiry
    BEKI Mnigeria wa Kagera Sugar, Benjamin Effe Ofuyah ameanza kuvitoa udenda vigogo vya soka Tanzania, Simba na Yanga kutokana na soka yake maridadi anayoonyesha katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Beki huyo wa kati aliwavutia Yanga walipokwenda Bukoba kucheza na Kagera Sugar Oktoba 8, katika mechi ambayo wenyeji walishinda 1-0, bao pekee la mkongwe Themi Felix kwenye Uwanja wa Kaitaba.
    Effe aliwavutia pia Simba katika mchezo wa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Kagera ikilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji wao.
    Effe ambaye anacheza kama sentahafu, akiwa pacha wa Amandus Nesta katika mechi na Simba alionyesha uwezo mkubwa wa kulinda na kusaidia mashambulizi.
    Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, kasi kuruka hewani kuicheza mipira kwa kichwa- nguvu za kupambana na washambuliaji na zaidi ni mtulivu, asiye na papara, mwenye maamuzi ya haraka.
    Mara kadhaa alishinda mipira dhidi ya washambuliaji hatari wa Simba, akina Mzambia Felix Mumba Sunzu Jr., Mganda Emmanuel Arnold Okwi na mzalendo Mrisho Khalfan Ngassa.
    Beki huyo amesajiliwa na Kagera Sugar kwa pamoja na mwenzake, mshambuliaji Wilfred Emmeh kutoka klabu ya Abuja FC ya kwao Nigeria. Kwa ujumla, katika kikosi cha Kagera kuna Wanigeria watatu, mwingine ni Enyinna Darlington ambaye amesajiliwa kutoka Toto African ya Mwanza, ambayo nayo ilimtoa Abuja FC ya Nigeria.  
    Kagera Sugar ni moja yenye timu zenye kusifika kwa kuvumbua vipaji, ambavyo baadaye vinanunuliwa kwa bei chafu na vigogo wa soka nchini, Simba, Yanga na hata Azam FC.
    Mrisho Ngassa, Amri Kiemba wa Simba, Said Mourad wa Azam FC, Godfrey Taita na David Luhende wa Yanga, wote hawa wametokea Kagera Sugar.
    Aidha, Kagera pia imekuwa ikiwarudisha wachezaji ambao wameonekana hawafai timu nyingine na kuwa na thamani tena, mfano Gaudence Exavery Mwaikimba aliyetupiwa virago Yanga akaenda kufufua makali yake huko, hatimaye kusajiliwa na Azam FC msimu uliopita.
    Salum Kanoni Kupela aliyetupiwa virago Simba SC hivi sasa anang’ara Kagera Sugar na ndiye aliyeifungia timu hiyo bao la kusawazisha kwa penalti katika mechi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, siku ambayo alionekana kumdhibiti vizuri Okwi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BEKI LA KAGERA LAZIMWAGA MATE SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top