• HABARI MPYA

    Wednesday, October 17, 2012

    SIMBA KUENDELEZA UBABE TAIFA LEO, AZAM INA KAZI KWA PRISONS SOKOINE

    Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    LIGI Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara, leo inaingia katika mzunguko wake wa nane kwa nyasi za viwanja vitano kuwaka moto, huku macho na masikio ya wengi yakielekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako mabingwa watetezi Simba watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera.
    Mechi hiyo namba 52 itachezeshwa na refa Ronald Swai kutoka Arusha, akisaidiwa na Julius Kasitu na Methusela Musebula, wote kutoka Shinyanga na refa wa akiba atakuwa Ephrony Ndisa wa Dar es Salaam.
    Kagera Sugar inayofundishwa na kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Abdallah Kibadeni mara nyingi imekuwa timu ambayo inaonyesha upinzani mkali inapokutana na Simba SC, iwe Dar es Salaam au Bukoba na leo inatarajiwa kuwa hivyo pia.
    Katika mchezo wa leo, huenda Simba ikaendelea kumkosa kiungo wake hodari, Mrisho Khalfan Ngassa ambaye pamoja na kuanza mazoeozi juzi na timu yake Simba SC, lakini amesema bado hayuko sawa sawa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY juzi, Ngassa ambaye aliugua Malaria baada ya mechi dhidi ya Yanga, Oktoba 3, mwaka huu alisema kwamba bado anahisi hana nguvu.
    “Nimeanza mazoezi na timu, lakini hata hivyo bado hali yangu haiko sawa sawa kwa kweli, najisikia mwili hauna nguvu, hii Malaria ilinipelekesha sana, ila najikongoza hivyo hivyo,”alisema Ngassa.
    Lakini kuna uhakika kwa kiungo mwingine wa Simba SC aliyekuwa anaumwa Malaria pia, Ramadhani Chombo ‘Redondo’  akacheza leo, kwa kuwa yeye yuko fiti asilimia 100.  
    Mbali na Redondo, katika mchezo huo, Simba inatarajiwa kuwapokea wachezaji wake wengine watatu iliyowakosa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ambayo iliisha kwa sare ya bila kufungana, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao Uganda kuichezea timu yake ya taifa, Komabil Keita, Haruna Shamte na Kiggi Makasy waliokuwa majeruhi.
    Mechi nyingine za leo Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale na Azam iliyo chini ya kocha Boris Bunjak kutoka Serbia. Nayo Polisi Morogoro iliyopanda msimu huu itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri.
    Mgambo Shooting ambayo imepata ushindi mara mbili mfululizo itakuwa nyumbani Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga ikiikaribisha Toto Africans katika mechi itakayochezeshwa na Geofrey Tumaini wa Dar es Salaam. Oljoro JKT inayonolewa na Mbwana Makata itakuwa nyumbani Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya African Lyon.
    Simba bado ipo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 17, baada ya kucheza mechi saba, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, ambayo hata hivyo imecheza mechi sita, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza mechi saba pia.

    REKODI YA SIMBA NA KAGERA:
    Machi 3, 2012
    Simba 3-1 Kagera Sugar
    Septemba 18, 2011
    Kagera Sugar 1-1 Simba
    Machi 29, 2011
    Simba 0-0 Kagera Sugar
    Oktoba 27, 2010
    Kagera Sugar 0-2 Simba
    Februari 3, 2010
    Kagera Sugar 1-1 Simba     
    Septemba 10, 2009
    Simba 2-0 Kagera Sugar
    Aprili 5, 2009
    Kagera Sugar 0-2 Simba 
    Oktoba 14, 2008
    Simba 1-0 Kagera Sugar  
    Aprili 19, 2008
    Kagera Sugar 0-1 Simba
    Oktoba 13, 2007
    Simba 2-1 Kagera Sugar
    Oktoba 18, 2006
    Simba 2-1 Kagera Sugar
    Juni 3, 2006
    Kagera Sugar 1-0 Simba
    (Kagera wakapewa ushindi wa mezani
    2-0, kwa Simba kumchezesha Mussa
    Mgosi akiwa ana kadi tatu za njano)
    Septemba 28, 2005
    Kagera Sugar 0-2 Simba    
    Mei 25, 2005
    Simba 0-1 Kagera Sugar
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA KUENDELEZA UBABE TAIFA LEO, AZAM INA KAZI KWA PRISONS SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top