• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2012

    TENGA ASEMA YANGA NA VODACOM WATAJUA WENYEWE

    Rais wa ^TFF, Leodegar Chilla Tenga (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari. Kulia kwake ni Sunday Burton Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na kushoto Katibu, Angetile Osiah Malabeja.

    Na Mahmoud Zubeiry
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba kwa sasa shirikisho lake linawaachia wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom watumie busara kumalizana na klabu ya Yanga, juu ya mgogoro wao kuhusu nembo ya ligi hiyo.
    Akijibu swali la BIN ZUBEIRY katika Mkutano wake maalum na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya TFF, kuzungumzia masuala ya uchaguzi wa vyama mbalimbali vya soka nchini, Tenga alisema kwamba kwa kuwa msimu uliopita Vodacom walimalizana na Yanga bila kulishirikisha shirikisho lake, na mwaka huu wanawaachia pia.
    “Kitendo kilichofanywa na Vodacom mwaka jana, kumalizana na Yanga bila kutushirikisha kuhusu utata wa nembo, sisi tulijua kitaleta matatizo baadaye, na kweli sasa yametokea, na ndiyo maana unaweza kuona, sekretarieti yetu inalipeleka taratibu hili suala,”alisema Tenga.
    Tenga alisema Vodacom ingewaacha TFF msimu uliopita wakaihukumu Yanga kwa mujibu wa kanuni, hata msimu huu ingekuwa rahisi kwao kuingilia, lakini kwa kuwa msimu uliopita waliingilia na wakaibadilishia klabu hiyo nembo, basi na msimu huu pia wanawaachia wamalizane wenyewe.
    Mwaka jana Yanga waligoma kuvaa jezi zenye nembo ya wadhamini wa Ligi Kuu, Vodacom kwa sababu zina nembo nyekundu hadi kampuni hiyo ikawabadilishia na kuwapa jezi maalum zenye nembo nyeusi.
    Mwaka huu pia, Yanga wamekataa kubandikiwa nembo za Vodacom kwenye jezi zao kwa sababu ya rangi hiyo nyekundu na jana wamecheza mechi ya sita bila kuvaa nembo ya mdhamini, wakisistiza wabadilishiwe.
    Wakati huo huo, kanuni za Ligi Kuu zinasema timu itakayogoma kuvaa nembo ya mdhamini itashushwa Daraja, ingawa tishio hilo la kanuni sasa linapozwa na kauli ya Tenga leo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TENGA ASEMA YANGA NA VODACOM WATAJUA WENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top