• HABARI MPYA

    Wednesday, October 17, 2012

    YANGA WAENDELEA VIZURI NA MAANDALIZI YA KUIUA RUVU SHOOTING JUMAMOSI

    Yanga SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIKOSI cha Yanga kilichoingia kambini jana katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar es Salaam kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Pamoja na kuweka kambi Changanyikeni, lakini Yanga inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
    Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, anaendelea vizuri na mazoezi mepesi sawa na mshambuliaji Said Bahanuzi aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
    Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Jumatatu wiki iliyopita.
    Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
    Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka. 
    Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11, baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
    Simba iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAENDELEA VIZURI NA MAANDALIZI YA KUIUA RUVU SHOOTING JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top