• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2012

    YANGA WAKANUSHA KULALA 'MZUNGU WA NNE' BUKOBA

    Mwalusako akizungumza na Waandishi wa Habari Jangwani leo

    Na Mahmoud Zubeiry
    KATIBU wa Yanga, Lawrence Mwalusako amesema kwamba timu yao ilifungwa kimchezo na labda kwa mbinu nyingine kwenye mechi ya jana dhidi ya Kagera Sugar, lakini si kwa sababu ya malazi mabaya wala lishe mbovu.
    Mwalusako aliyezungumza na Waandishi wa Habari ‘hivi punde’ makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, alikuwa anakanusha habari zilizoandikwa na gazeti moja leo, kwamba wachezaji wake walilala wawili wawili kitanda kimoja mjini Bukoba.
    “Hizi habari si kweli, wachezaji wetu walilala vizuri tu, tunasikitishwa na habari za kizushi kama hizi, tunapenda kukanusha kwa nguvu zote,”alisema.
    Mwalusako alisema kufungwa kwao Kagera kumetokana na matokeo ya kawaida ya mchezo na sasa kuelekea mechi ya Alhamisi dhidi ya Toto African mjini Mwanza wataongeza nguvu.
    “Kuna viongozi wataenda Mwanza kuongeza nguvu, ili kuhakikisha tunashinda mechi hiyo, wanakwenda kwa ajili ya kuwahamasisha wachezaji,”alisema Mwalusako.  
    Bao pekee la Themi Felix katika dakika ya 67, jana liliwapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
    Hiyo inakuwa mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo Simba SC.
    Aidha, hii ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.  
    Kwa ujumla Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa, ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na jana imechapwa 1-0 na Kagera Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
    Katika mechi hiyo ya jana, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
    Tangu ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya hayo kwa penalti.  

     Mchezaji wa yanga Oscar Joshua akiwa ndani ya chumba chake.
     Wachezaji wa timu ya Yanga, Omega Seme kulia na Frank Domayo kushoto wakiwa wamejipumzisha ndani ya vyumba vyao. Je, huu ni mzungu wa nne?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAKANUSHA KULALA 'MZUNGU WA NNE' BUKOBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top