• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2012

    YANGA WAKIGARAGAZA TENA KIDOA CHEKUNDU CHA VODA, WAPEWA VIDOA VIPYA VITATU WACHAGUE






    Na Prince Akbar
    WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom Tanzania, wameikubalia klabu ya Yanga kutotumia jezi zenye nembo nyekundu na kuipa nembo tatu ichague mojawapo, ambazo hazina rangi nyekundu.
    Nembo hizo ni njano na nyeusi, kijani na nyeusi na nyeupe na nyeusi, ambazo Yanga itatakiwa kuchagua mojawapo kutumia katika Ligi Kuu.
    Yanga walikuwa wana mgomo wa kutumia nyembo nyekundu, ambayo ndio nembo kuu ya kampuni hiyo kwa sasa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga akasema wanawaachia Vodacom watumie busara kumalizana na klabu ya Yanga, juu ya mgogoro wao kuhusu nembo ya ligi hiyo.
    Tenga alisema kwamba kwa kuwa msimu uliopita Vodacom walimalizana na Yanga bila kulishirikisha shirikisho lake, na mwaka huu wanawaachia pia.
    “Kitendo kilichofanywa na Vodacom mwaka jana, kumalizana na Yanga bila kutushirikisha kuhusu utata wa nembo, sisi tulijua kitaleta matatizo baadaye, na kweli sasa yametokea, na ndiyo maana unaweza kuona, sekretarieti yetu inalipeleka taratibu hili suala,”alisema Tenga.
    Tenga alisema Vodacom ingewaacha TFF msimu uliopita wakaihukumu Yanga kwa mujibu wa kanuni, hata msimu huu ingekuwa rahisi kwao kuingilia, lakini kwa kuwa msimu uliopita waliingilia na wakaibadilishia klabu hiyo nembo, basi na msimu huu pia wanawaachia wamalizane wenyewe.
    Hatua hiyo ya Vodacom kuibadilishia Yanga nembo ya jezi, inakuja siku mbili baada ya Wazee wa klabu hiyo, kutoa tamko la kusema wapo tayari klabu hiyo ishushwe daraja kwa mujibu wa kanuni, lakini si kuvaa nembo nyekundu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAKIGARAGAZA TENA KIDOA CHEKUNDU CHA VODA, WAPEWA VIDOA VIPYA VITATU WACHAGUE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top