• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2012

    RUVU SHOOTING NA YANGA KUCHEZA TAIFA KESHO, MECHI ZOTE ZA AZAM NA SIMBA NA YANGA KUCHEZWA TAIFA PIA

    Ruvu Shooting; Wenyeji mechi ya kesho

    Na Prince Akbar
    MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliopangwa kuchezwa kesho Uwanja wa Chamazi, sasa umehamishiwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mabadiliko hayo yamefanyika kutokana na maombi ya timu hizo mbili kutaka mechi ichezwe Uwanja wa Taifa kutokana na sababu mbalimbali ambazo zimeridhiwa na Kamati ya Ligi ya TFF, ikiwemo siku hiyo uwanja huo kutokuwa na mechi.
    Wambura amesema katika mechi hiyo, itakayochezeshwa na refa Amon Paul kutoka Mara ni viingilio vitakuwa Sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, Sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, Sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
    Amesema pia, Kamati ya Ligi imekataa ombi la timu ya Azam kutaka mechi zake za nyumbani za ligi hiyo zichezwe dhidi ya Simba na Yanga zichezwe Uwanja wa Chamazi kutokana na sababu za kiusalama.
    Mechi nyingine za kesho, Coastal Union itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambayo itachezeshwa na refa Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote kutoka Dar es Salaam.
    Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili kwa mechi tatu, JKT Ruvu itaonyeshana kazi na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RUVU SHOOTING NA YANGA KUCHEZA TAIFA KESHO, MECHI ZOTE ZA AZAM NA SIMBA NA YANGA KUCHEZWA TAIFA PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top