• HABARI MPYA

    Sunday, November 18, 2012

    KILA LA HERI SERENGETI BOYS, TWENDENI TUKAWAPE SAPOTI VIJANA TAIFA LEO

    Wachezaji wa Serengeti Boys wakiomba dua kabla ya mazoezi yao Alhamisi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

    Na Mahmoud Zubeiry
    TIMU ya ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na vijana wenzao, Kongo Brazzaville katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Tatu nay a mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini Morocco mwakani.
    Serengeti wanaingia kwenye mchezo huo, wakiwa na matumaini makubwa ya ushindi kutokana na maandalizi mazuri waliyopewa.
    Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Mdenmark Jacob Michelsen amesema ana matumaini ya ushindi katika mchezo huo kutokana na maandalizi mazuri, ingawa amesema anaa wasiwasi wapinzani wake wana wachezaji waliozidi umri.
    Michelsen alisema kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina ya Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya wapinzani wao.
    Pamoja na kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
    “Nilipokwenda kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa miaka 15.
    Mimi ni kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za U17 una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya wachezaji anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
    Amesema wamecheza mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na hawajafungwa hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
    Nahodha wa Serengeti Boys, Miraj Adam amesema leoo watapigana kwa nguvu zao zote, kuhakikisha wanawafunga Kongo Brazzaville ili watimize ndoto zao za kucheza Fainali za Morocco mwakani.
    Adam alisema kwamba hata kama Kongo Brazzaville wamekuja na wachezaji waliovuka umri kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, lakini kesho watafungwa tu.
    “Kongo watakufa, watake wasitake, nasema Kongo watakufa,”alisema.
    Kwa upande wake, Msaidizi wake, Hussein Twaha ‘Messi’ alikumbushia maneno waliyoambiwa na mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele katika ziara yake nchini hivi karibuni na kusema yatakuwa kichocheo kwao kufanya vizuri na kukata tiketi ya Morocco.
    “Pele alituambia mpira unachezwa na watoto kutoka familia masikini, hata yeye alitoka familia ya kimasikini, akajitahidi akafanikiwa na kufanya watoto wake waingie katika mpira wakitokea familia ya kitajiri, hivyo na sisi tunatumia kauli hii kama kichocheo cha kufanya vizuri ili tufuate nyayo zake,”alisema Twaha.
    Serengeti imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu hii itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
    Hata hivyo, pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KILA LA HERI SERENGETI BOYS, TWENDENI TUKAWAPE SAPOTI VIJANA TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top