Searching...
Tuesday, November 20, 2012
11/20/2012 06:35:00 AM

NIYONZIMA, KAVUMBANGU KWAHERI YANGA

Haruna Niyonzima anakwenda El Merreikh

Na Mahmoud Zubeiry
KLABU ya Yanga imepokea ofa kutoka klabu mbili tofauti, moja ya Asia na moja ya hapa hapa Afrika zikiwahitaji wachezaji wao mahiri wa kigeni, kiungo Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na mshambuliaji Didier Kavumbangu kutoka Burundi.
Habari za ndani kutoka Yanga, zimesema kwamba, Niyonzima anatakiwa na klabu ya El Merreikh ya Sudan, wakati Kavumbangu anatakiwa na klabu moja ya Qatar.   
Tayari barua rasmi za kuwahitaji wachezaji hao zimekwishawasilishwa Yanga na hivi sasa klabu inaingia kwenye majadiliano ya bei na klabu hizo.
Klabu ya Qatar, ilitangaza ofa ya dola za Kimarekani 100,000 (zaidi ya Sh. Milioni 150), lakini Yanga imekataa dau hilo na inataka dola 300,000 (zaidi ya Sh. Milioni 450) kwa ajili ya Kavumbangu.
Kuhusu Niyonzima, Merreikh imeomba itajiwe bei ya mchezaji huyo na Yanga. “Merreikh wana fedha, hatuna wasiwasi nao, sisi tutaanzia dola 300,000 na hata tukishuka, si chini ya 200,000, hawa wachezaji ni lulu”kilisema chanzo kutoka Yanga.
Didier Kavumbangu anakwenda Qatar
Haruna alisajiliwa msimu uliopita Yanga kutoka APR ya Rwanda, wakati Kavumbangu amesajiliwa msimu huu kutoka Atletico Olympic ya Burundi.
Kavumbangu kwa sasa ndiye anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiwa ametikisa nyavu mara nane, sawa na Kipre Tcheche wa Azam FC.
Wataalamu wa usajili wa Yanga, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Ahmad ‘Bin Kleb’ tayari wanajiandaa kwenda Kampala, Uganda itakapofanyika michuano ya Kombe la Challenge kutafuta wachezaji wa kuziba nafasi za Kavumbangu na Niyonzima.
Lakini habari zaidi zinasema nafasi ya Niyonzima itazibwa na Kabange Twite kutoka APR ya Rwanda, ndugu wa mchezaji mwingine wa Yanga, Mbuyu Twite.  

 
Back to top!