• HABARI MPYA

    Saturday, November 17, 2012

    WACHEZAJI SERENGETI WASEMA, HATA KAMA WAMEKUJA NA VIBABU, KONGO LAZIMA WAFE KESHO TAIFA

    Miraj Adam kulia akizungumza jana na kushoto ni Hussein Twaha

    Na Mahmoud Zubeiry
    NAHODHA wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, Miraj Adam amesema kesho watapigana kwa nguvu zao zote, kuhakikisha wanawafunga Kongo Brazzaville ili watimize ndoto zao za kucheza Fainali za Vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini Morocco mwakani.
    Akizungumza jana kwenye hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam, Adam alisema kwamba hata kama Kongo Brazzaville wamekuja na wachezaji waliovuka umri kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, lakini kesho watafungwa tu.
    “Kongo watakufa, watake wasitake, nasema Kongo watakufa,”alisema kwa hisia kali Adam anayechezea Simba wakati wa hafla maalum ya chakula cha usiku kuichangia timu hiyo.
    Kwa upande wake, Msaidizi wake, Hussein Twaha ‘Messi’ alikumbushia maneno waliyoambiwa na mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele katika ziara yake nchini hivi karibuni na kusema yatakuwa kichocheo kwao kufanya vizuri na kukata tiketi ya Morocco.
    “Pele alituambia mpira unachezwa na watoto kutoka familia masikini, hata yeye alitoka familia ya kimasikini, akajitahidi akafanikiwa na kufanya watoto wake waingie katika mpira wakitokea familia ya kitajiri, hivyo na sisi tunatumia kauli hii kama kichocheo cha kufanya vizuri ili tufuate nyayo zake,”alisema Twaha, anayechezea Coastal Union.
    Kocha Mkuu, Mdenmark Jacob Michelsen alishukuru kwa sapoti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika maandalizi na akasema ana matumaini makubwa ya kuwatoa Kongo, kwani amewaandaa vema vijana wake.
    Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema kwamba wachezaji wanatakiwa kujituma ili kushinda mechi hiyo na kujiwekea mazingira mazuri ya kufuzu.
    Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia vijana kwamba amekuwa mchezaji, kocha, kiongozi, Mjumbe wa bodi mbalimbali na Mwenyekiti wa Bodi, lakini katika maisha yake ya soka hakuna kitu anachojivunia kama kuwa Nahodha wa timu ya taifa, hivyo akawataka vijana wakapigane kesho kwenda kuweka historia.
    Juzi Michelsen alisema kwamba ana wasiwasi wapinzani wake, Kongo Brazzaville wana wachezaji waliozidi umri, baada ya kuichunguza vizuri Kongo na sasa anaifahahamu vema.
    Michelsen alisema kwamba alikwenda kushuhudia mchezo wa kwanza wa raundi iliyopita, baina ya Kongo na Zimbabwe waliotolewa na wapinzani wao hao na kujionea makali ya wapinzani wao.
    Pamoja na kukiri kwamba Kongo ni timu bora na ilicheza Fainali zilizopita za Kombe la Dunia nchini Mexico mwaka jana na kutolewa raundi ya pili, Michelsen alisema bado ana wasiwasi timu hiyo ina ‘vijeba’.
    “Nilipokwenda kuwaangalia wakicheza na Zimbabwe, nilikuta kikosini mwao kuna wachezaji sita wa kikosi kilichokwenda Mexico kwenye Kombe la Dunia, inanitia shaka kwa sababu hakuna mchezaji anayeweza kucheza michuano mikubwa kama ile akiwa ana umri wa miaka 15.
    Mimi ni kocha wa vijana na ninajua, haiwezekani. Ucheze fainali za Kombe la Dunia za U17 una miaka 15, hakuna,”alisema Michelsen, ambaye aliwataja baadhi ya wachezaji anaowatilia shaka wamezidi umri ni Hady Binguila na Charvely Mabiat.
    Amesema wamecheza mechi za kujipima nguvu 15 zikiwemo dhidi ya timu za Ligi Kuu na hawajafungwa hata moja, kitu ambacho anaamini ni kipimo cha ubora wa timu yake.
    Serengeti jana ilihamia katika hoteli ya JB Belmonte, kutoka hoteli ya Itumbi, ili kuwaweka vizuri kisaikolojia vijana, hizo zikiwa ni jitihada za Kamati maalum iliyoundwa kuisaidia timu hiyo. 
    Serengeti imefanikiwa kufuzu hadi Raundi ya Tatu bila jasho, baada ya wapinzani wake wa awali katika Raundi ya Kwanza na ya Pili, Kenya na Misri kujitoa. Iwapo timu hii itafuzu, hii itakuwa mara ya pili kwa Serengeti kukata tiketi ya kucheza fainali hizo, baada ya mwaka 2005.
    Hata hivyo, pamoja na kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe, Serengeti haikwenda Gambia mwaka huo kutokana na kuondolewa kwenye michuano hiyo na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kubainika walitumia kijana aliyezidi umri, Nurdin Bakari.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WACHEZAJI SERENGETI WASEMA, HATA KAMA WAMEKUJA NA VIBABU, KONGO LAZIMA WAFE KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top