• HABARI MPYA

    Thursday, November 01, 2012

    WACHEZAJI YANGA WAPO BAGAMOYO, BRANDTS ANAIFANYIA USHUSHUSHU AZAM CHAMAZI

    Brandts akiwa Uwanja wa Chamazi mida hii

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC leo imeingia kambini katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani Pwani kujiandaa na mchezo wake wa Jumapili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Jumapili, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa kawaida, Yanga huweka kambi Bagamoyo katikati ya Ligi, inapokuwa inajiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC hivyo kwa kwenda huko kuweka kujiandaa na mchezo huo, maana yake wanaupa uzito sawa na pambano la watani.
    Wakati vijana wa Yanga wakiwa Bagamoyo, Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi Ernie Brandts yupo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, akiwafanyia ‘ushushushu’ wapinzani wake hao wanaomenyana na Coastal Union ya Tanga mida hii, kipindi cha kwanza wakiwa wanaongoza 3-0.    
    Brandts jana aliiongoza Yanga SC kuendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa Mgambo JKT ya Handeni, Tanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Yanga sasa iwe na pointi sawa na mabingwa watetezi, Simba SC waliotoa sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro leo, ingawa inazidiwa bao moja tu katika wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
    Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Didier Kavumbangu.
    Cannavaro alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Oscar Joshua dakika ya pili kutoka wingi ya kulia, wakati Kavumbangu alimalizia pasi ya Hamisi Kiiza dakika ya 39.
    Pamoja na kutoka uwanjani wamelowa kipindi cha kwanza, lakini Mgambo JKT walicheza soka ya kuvutia na mara mbili walikaribia kufunga kupitia kwa Juma Mwinyimvua.
    Yanga walicheza vema dakika 45 za kipindi cha kwanza, tofauti sana na mechi za awali ambazo wamekuwa ‘wakichezewa’ sana na wapinzani.
    Ilishuhudiwa katika kipindi hicho, Yanga wakimiliki zaidi mpira na kupeana pasi za uhakika, ingawa mashambulizi yao mengi walipitisha pembeni, hasa upande wa kulia.
    Hamisi Kiiza, Msuva na Kavumbangu walicheza kwa uelewano mkubwa pale mbele na kulitia misukosuko haswa lango la Mgambo. 
    Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto wao tena na kuendelea kuwachachafya Mgambo.
    Hata hivyo, iliwachukua Yanga dakika 34 kupata bao la tatu, mfungaji akiwa ni Jerry Tegete aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya Kavumbangu.
    Tegete alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya beki wa kushoto, Oscar Joshua.
    Pamoja na kufungwa, Mgambo waliendelea kusukuma mashambulizi langoni mwa Yanga, ingawa leo mabeki wa timu hiyo, inayofundishwa na Mholanzi, Ernie Brandts walicheza kwa uelewano mkubwa na kudhibiti hatari zote langoni mwao. 
    Mgambo inayofundishwa na Mohamed Kampira, ilipata pigo dakika ya 85, baada ya beki wake wa kulia, Salum Mlima kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea rafu mbaya Mbuyu Twite. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA WAPO BAGAMOYO, BRANDTS ANAIFANYIA USHUSHUSHU AZAM CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top