• HABARI MPYA

    Thursday, December 06, 2012

    NGASSA: SIMBA PANDENI DAU NIBAKI MSIMBAZI

    Mrisho Ngassa

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    MRISHO Khalfan Ngassa amesema kama Simba wanampenda sana, wapande dau walilotoa El Merreikh ili aghairi kwenda Sudan.
    Akizungumza hapa, Ngassa alisema kwamba yeye kama mchezaji anaangalia maslahi na kwa mshahara mzuri pamoja na dau nono la usajili alilopewa Matajiri wa Sudan amelainika na kukubali kujiunga nayo. 
    Wakati Azam FC imemuuza Ngassa kwa dola za Kimarekani 75,000 kwenda El Merreikh ambako amesaini mkataba wa miaka miwili, kiungo huyo mshambuliaji amepewa dau la kusaini mkataba wa miaka miwili, dola 50,000 na atakuwa analipwa mshahara wa dola 4,000 kwa mwezi.
    Awali, Merreikh walitaka kumpa mkataba wa miaka mitatu Ngassa wenye thamani ya dola 100,000, lakini wakala wake Alhaj Yussuf Said Bakhresa akakataa akisema utambana mchezaji wake aking’ara na kutakiwa na klabu nyingine.
    Sasa Ngassa baada ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwishoni mwa wiki hii, atakwenda Sudan kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na klabu hiyo, ambayo ni jambo la kawaida kucheza hatua ya makundi ya michuano ya klabu Afrika.
    Azam FC imesema imeweka mbele maslahi ya mchezaji na taifa kwa ujumla katika maamuzi ya kumuuza Sudan, kutoka Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo. “Hii timu (Merreikh) kila mwaka inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, maana yake huyu mchezaji atakwenda kupata maendeleo na kuja kuisaidia zaidi Tanzania katika mashindano ya kimataifa,”alisema kiongozi mmoja wa Azam. 
    Alipoulizwa kuhusu Simba SC aliyokuwa anaichezea klabu hiyo, kiongozi huyo alisema wao walimtoa kwa mkopo Ngassa kwenda kwa Wekundu wa Msimbazi hadi Mei 31, mwakani na mkataba wao ndio unasema hivyo.
    “Sisi tuliwapa Simba huyu mchezaji kwa mkopo hadi Mei 31 na wakatupa Sh. Milioni 25, ila tuko tayari kuwarudishia fedha zao walizota, lakini huyu mchezaji ni mali yetu  na hata TFF wa natambua hilo, na tumekwishamuuza Merreikh,”alisema.
    Alipoulizwa kuhusu Simba kusaini mkataba mpya na Ngassa, alisema; “We uliona wapi dunia nzima timu inapewa mchezaji kwa mkopo halafu inamsainisha mkataba? Simba lazima ifike wakati waache kurudia makosa, haya ndio mambo ya Mbuyu Twite sasa,”alisema kiongozi huyo wa Azam.
    Azam walimtoa kwa mkopo Ngassa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu baada ya kukerwa na kitendo cha mchezaji huyo kubusu jezi ya timu yake ya zamani, Yanga, katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Alifanya hivyo, baada ya kufunga bao la ushindi akitokea benchi na kuiwezesha Azam kutinga fainali ya michuano hiyo, ambako walifungwa na Yanga 2-0, naye kwa mara nyingine akitokea benchi na kushindwa kufunga, hivyo kutuhumiwa kucheza kinazi.
    Ilielezwa kwamba Simba walitoa Sh. Milioni 25 kumnunua kwa mkopo mchezaji huyo, ingawa baadaye Simba wakasema waliununua mkataba wa mwaka mmoja aliobakiza mchezaji huyo Azam FC, nao wakamuongezea wa mwaka mmoja kwa kumsainisha kwa Sh. Milioni 30, kati ya hizo Milioni 12 akipewa taslimu na 18 akipewa gari.
    Ngassa anang’ara katika Challenge ya mwaka huu mjini hapa, hadi sasa akiwa amefunga mabao matano sawa na John Bocco wa Azam na wafungana kileleni.

    WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
    John Bocco                   Tanzania  5
    Mrisho Ngassa              Tanzania  5
    Brian Umony                 Uganda    3
    Suleiman Ndikumana    Burundi    3 (1 penalti)
    Chris Nduwarugira        Burundi    3
    Geoffrey Kizito              Uganda     2
    Robert Ssentongo         Uganda    2
    Khamis Mcha                Zanzibar   2
    David Ochieng              Kenya       2
    Clifton Miheso               Kenya       2
    Dadi Birori                     Rwanda    2
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NGASSA: SIMBA PANDENI DAU NIBAKI MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top