• HABARI MPYA

    Wednesday, December 05, 2012

    POULSEN AFICHUA SIRI YA KUMPIGA BENCHI MSUVA

    Kim Poulsen kulia na Msaidizi wake Marsh kushoto

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema kwamba anamuweka benchi kwa sasa kiungo mshambuliaji Simon Msuva, katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, kwa sababu Amri Kiemba anafanya kazi nzuri katika kikosi cha kwanza.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mahojiano maalum jana, Uwanja wa Mandela, Namboole, alisema kwamba alipompa nafasi ya Kiemba amefanya kazi nzuri ambayo imemvutia na kuamua kuendelea kumtumia kwenye kikosi cha kwanza.
    “Najua Msuva ni winga mzuri, ana kasi na anashambulia sana, lakini hata Kiemba anafanya kazi nzuri, tena kama jana (juzi) amefunga hadi bao, kwa kweli ananivutia na anafanya kazi yake vizuri,”alisema.
    Msuva alianza katika mechi mbili za mwanzoni za Kundi B kwenye michuano hii, dhidi ya Sudan na Burundi, lakini baada ya hapo amemalizia benchi dakika zote 180 katika mechi kwenye mechi mbili zilizofuata dhidi ya Somalia na Rwanda. 
    Hata hivyo, Kim alisema bado Msuva anaweza akatokea benchi wakati wowote na kwenda kuongeza nguvu katika kikosi cha Kilimanjaro Stars hasa katika hatua ngumu ambayo michuano hii imefikia.
    Stars imefika Nusu Fainali na kesho itamenyana na wenyeji Uganda, Uwanja wa Mandela, Namboole, kuanzia saa 12: jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali nyingine kati ya Kenya na Zanzibar, itakayoanza saa 10:00 jioni.
    Stars ilitinga Nusu Fainali, baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 juzi kwenye Uwanja wa Lugogo mjini hapa, ambayo yalitiwa kimiani na Amri Kiemba na John Bocco.
    Awali ya hapo, Stars ilifuzu Robo Fainali kama mshindi wa pili kwenye kundi lake, nyuma ya Burundi baada ya kujikusanyia pointi sita, yaani ikishinda mechi mbili 2-0 na Sudan na 7-0 na Somalia, wakati yenyewe ilifungwa 1-0 Mbayuwayu wa Bujumbura. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: POULSEN AFICHUA SIRI YA KUMPIGA BENCHI MSUVA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top