• HABARI MPYA

    Sunday, April 13, 2014

    AZAM BINGWA LIGI KUU, YAICHAPA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE

    Na Mahmoud Zubeiry, Mbeya
    AZAM FC ndiye bingwa mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini hapa, huku waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC wakishinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro mjini Arusha leo. 
    Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho Aprili 19, mwaka huu.
    Gaudence Mwaikimba akishangilia baada ya kuifungia Azam bao la kwanza, Kulia ni Kipre Tchetche

    Yanga SC yenye pointi 55 sasa ikiifunga Simba SC Aprili wiki ijayo itafikisha 58.
    Mabao ya Azam leo yamefungwa na Gaudence Mwaikimba na John Bocco, wakati la Mbeya City limefungwa na Mwagane Yeya. 
    Mchezo ulikuwa mkali na ulianza kwa kasi timu zote zikishambuliana kwa zamu, na sifa ziwaendee makipa wa timu zote mbili, David Burhan wa Mbeya City na Aishi Manula wa Azam FC kwa kazi nzuri ya kuokoa hatari langoni mwao.
    Azam walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 43, mfungaji Gaudence Mwakimba aliyemalizia pasi nzuri ya beki wa kulia Erasto Nyoni.
    Baada ya bao hilo, Mbeya City walicharuka na kufanya mashambulizi mawili hatari langoni mwa Azam, lakini hawakuweza kupata bao hadi kipyenga cha kuhitimisha kipindi cha kwanza kinapulizwa.
    Kipindi cha pili, Azam waliingia na mfumo wa kucheza kwa kujihami ili kulinda bao lao, mbele wakimuacha Mwaikimbe pekee na John Bocco akashuka katikati huku Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akimsaidia Kipre Balou kukaba kiungo cha chini.
    Mfumo huo ulikabirisha mashambulizi mengi langoni mwa Azam na haikuwa ajabu Mbeya City walipokomboa bao dakika ya 70 kupitia kwa Mwagane Yeya baada ya kuuwahi mpira uliopanguliwa na kipa Aishi Manula kufuatia shuti la Deus Kaseke.
    Bao hilo kidogo liliwachanganya Azam FC na Mbeya City wakauteka mchezo kwa dakika kadhaa, kabla ya shambulizi la kushitukiza kuipa ushindi timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa dakika ya 86, baadaa ya John Bocco kukutana na mpira uliorudishwa.
    Wachezaji wa Mbeya City walimzonga refa Nathan Lazaro wa Kilimanjaro baada ya bao hilo na kusababisha mchezo kusimama kwa zaidi ya dakika tatu.
    Refa huyo alitoa kadi nyekundu kwa Mwagane Yeya baada ya vurugu hizo. Askari wa jeshi la Polisi walilazimika kufanya kazi ya ziada baada ya mechi kwa kuwadhibiti mashabiki wa Mbeya City waliotaka kufanya vurugu na pia kuusindikiza msafara wa Azam FC.
    Pamoja na kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake leo, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo
    Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Afrucans 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
    Kikosi cha Mbeya City leo kilikuwa; David Burhan, Aziz Sibo/Hamad Kibopile dk50, Hassan Mwasapili, Yussuf Abdallah, Yohana Morris, Anthony Matogolo, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga, Saad Kipanga/Alex Sethi dk68 na Deus Kaseke. 
    Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Said Mourad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar, Gaudence Mwaikimba, John Bocco na Kipre Tchetche/Kevin Friday dk51.
    Katika mechi nyingine za ligi hiyo leo, Ashanti United imeilaza Simba SC 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la Mohamed Nampaka dakika ya 17, Yanga SC imeifunga JKT Oljoro 2-1 mabao yake yakifungwa na Rajab Zahir dakika ya 70 na Mrisho Ngassa dakika ya 73 huku la wenyeji likifungwa na Jacob Masawe dakika ya 68.
    Bao pekee la Elias Maguri dakika ya 36 limeizamisha Mtibwa Sugar 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, wakati Mgambo JKT imelazimishwa sare ya bila kufungana na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM BINGWA LIGI KUU, YAICHAPA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top