• HABARI MPYA

    Wednesday, April 16, 2014

    YANGA SC WAINGIA KAMBINI KAWE BEACH BILA OKWI

    Na Dina Ismail, Dar es Salaam
    YANGA SC imeingia kambini katika hoteli moja jirani ya Kawe Beach, Dar es Salaam kujiandaa na pambano dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC imerejea leo Dar es Salaam, ikitokea Moshi mkoani Kilimanjaro ambako jana ilicheza mechi ya kirafiki ikitokea Arusha katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Oljoro.
    Yanga iliyoifunga Panone ya Kilimanjaro mabao 3-0 jana wafungaji Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hussein Javu imeingia kambini bila mshambuliaji wake Emmanuel Okwi ambaye hajacheza mechi tatu zilizopita.
    Emmanuel Okwi hayupo kambini Yanga SC


    Mchezo huo wa kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unakuja wakati bingwa amekwishapatikana ambaye ni Azam FC na mshindi wa pili kadhalika, ambaye ni Yanga.
    Mchezo wa Jumamosi ni muhimu kwa Yanga SC kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 na Simba SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Desemba 21, mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kipigo cha Desemba kiliifanya Yanga SC ikavunja benchi lake zima la Ufundi kwa kuwafukuza makocha Mholanzi, Ernie Brandts na Wasaidizi wake Freddy Felix Minziro na Razack Ssiwa, ikiwaajiri Mholanzi mwingine, Hans van der Pluijm, Charles Boniface Mkwasa na Juma Nassor Pondamali.   
    Benchi jipya la Ufundi Yanga SC baada ya kuikosesha timu ubingwa, sasa linakabiliwa na mtihani mwingine wa kurejesha heshima mbele ya watani wao, Simba SC Jumamosi.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAINGIA KAMBINI KAWE BEACH BILA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top