• HABARI MPYA

    Wednesday, July 16, 2014

    LOGA ATAJA WATATU WAPYA ANAOWATAKA SIMBA SC IWE TISHIO MSIMU UJAO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mcroatia Zdravko Logarusic amesema kwamba anahitaji wachezaji wapya watatu wa kimataifa katika kikosi chake, beki, kiungo mkabaji na mshambuliaji ili awe na timu bora ya ushindani.
    Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY juzi mjini Dar es Salaam, kocha huyo wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya amesema kwamba anahitaji wachezaji hao, wenye uzoefu ambao atawaunganisha na alio nao ili kuwa na Simba bora.
    “Hakika ninahitaji wachezaji wenye sifa za kimataifa, nahitaji beki mmoja, kiungo wa ulinzi na mshambuliaji, ili niwaunganishe na nilionao kupata kikosi bora,”amesema.
    Loga amesema kwamba tayari amekwishawaambia viongozi wa klabu hiyo juu ya hilo na wiki hii atakuwa na kikao nao kujadili zaidi juu ya suala hilo.
    Nataka wazoefu; Logarusic kushoto akizungumza na Mtendaji Mkuu wa BIN ZUBEIRY Blog, Mahmoud Zubeiry kulia  

    Simba SC imeanza rasmi mazoezi juzi Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), eneo la Mlimani Dar es Salaam na Logarusic hajaridhishwa sana na hali ya Uwanja wanaotumia kwa sasa.
    “Kocha lazima hawezi kufurahishwa na Uwanja huu, tunahitaji Uwanja bora zaidi kwa maandalizi mazuri, tunajikusanya hapa kwa sasa, nadhani wiki ijayo tutakwenda kuanza maandalizi rasmi Zanzibar, huko naamini tutapata Uwanja mzuri,”alisema.
    Kuhusu baadhi ya wachezaji wapya chipukizi waliosajiliwa, Loga amesema wanatakiwa kujituma ili kufikia kiwango cha kimataifa, kwa sababu Simba SC ni timu kubwa na wao lazima waonyeshe uwezo mkubwa.
    “Wametoka timu ndogo ndogo na wana vipaji, lakini wanatakiwa kufanya bidii hapa, kwa sababu Simba ni timu kubwa, lazima waonyeshe uwezo wa kimataifa,”amesema.
    Loga amesema kwa kuwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaanza Septemba 20 anaamini ana muda wa kutosha wa maandalizi kuanzia sasa.
    Loga aliingia Simba SC Desemba mwaka jana akitokea Gor Mahia ya Kenya na mwisho wa msimu, akaamaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Mbeya City.
    Baada ya matokeo hayo mabaya, Mcroatia huyo sasa amepania kuwa na timu imara ya kushinda mataji msimu ujao, akizingatia upinzani mkali kutoka kwa mabingwa watetezi, Azam FC, washindi wa pili, Yanga SC na washindi wa tatu Mbeya City.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LOGA ATAJA WATATU WAPYA ANAOWATAKA SIMBA SC IWE TISHIO MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top