• HABARI MPYA

    Monday, July 14, 2014

    MBRAZIL SANTOS ANATUA KESHO DAR KUFANYA MAJARIBIO YANGA SC, AKIFUZU TU, OKWI ANATUPIWA VIRAGO AKAWASUMBUE NA WENGINE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Geilson Santana Santos ‘Jaja’ kutoka Brazil anatarajiwa kuwasili kesho mchana kwa ajili ya kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam. 
    BIN ZUBEIRY inafahamu Jaja ameondoka Brazil jana usiku na kesho mchana atakuwa Dar es Salaam tayari kujaribu bahati yake kwa timu hiyo ya Jangwani.
    Jaja anakuja Yanga SC kufanya majaribio na kama kocha Mkuu, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo atamkubali, atafanyiwa vipimo vya afya ambavyo akifaulu pia atasajiliwa.
    Na Yanga SC inataka kumuengua mshambuliaji Mganda, Emmanual Okwi katika usajili wake ili Mbrazil huyo achukue nafasi.
    Jaja atatua kesho Dar es Salaam

    Yanga inaamua kuachana na Okwi kwa sababu inaamini ni msumbufu na usajili wake uligubikwa na ‘magumashi’ nyingi zilizofanywa na viongozi wa klabu hiyo walioshughulikia suala lake, jambo ambalo limemkera Mwenyekiti Yussuf Manji.
    Yanga SC ina wachezaji watano wa kigeni kwa sasa bila ya Jaja na kabla ya kumtema Okwi, wengine wakiwa ni beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima wote wa Rwanda, Hamisi Kiiza na Coutinho.
    Jaja aliyezaliwa Septemba 21 mwaka 1985 (Miaka 28) mjini Aracaju, Brazil anatokea klabu ya Itabaiana aliyojiunga nayo mwaka 2006 na kabla ya hapo alichezea klabu za Coritiba, Catuense, Olimpico, zote mwaka 2013, Maruinense, Lagarto mwaka 2012, Olimpico tena 2011, Domingos 2010, Confianca 2008 na Sergipe 2007.
    Mbali na Maximo na Coutinho, kocha Msaidizi wa Yanga SC, Leonardo Neiva pia ni Mbrazil ambao wote wanaingia msimu huu.
    Maximo si mgeni Tanzania, kwani kati ya mwaka 2006 na 2010 alikuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars kabla ya kujiuzulu na kurejea kwao, nafasi yake ikichukuliwa na Mdenmark, Jan Poulsen aliyempisha nduguye, Kim Poulsen ambaye naye ameondolewa na kuajiriwa Mholanzi, Mart Nooij.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBRAZIL SANTOS ANATUA KESHO DAR KUFANYA MAJARIBIO YANGA SC, AKIFUZU TU, OKWI ANATUPIWA VIRAGO AKAWASUMBUE NA WENGINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top