• HABARI MPYA

    Thursday, August 21, 2014

    JAJA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO YANGA SC IKIIADHIBU ‘KISHIKAJI’ CHIPUKIZI YA PEMBA

    Na Mwandishi Wetu, PEMBA
    MSHAMBULIAJI Mbrazil, Geilson Santana ‘Jaja’ amefunga bao lake la kwanza akiichezea mechi yake ya kwanza, timu yake mpya, Yanga SC ikiibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Chipukizi Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba. 
    Jaja alifunga bao hilo dakika ya sita kwa kichwa akimalizia kona ya Haruna Niyonzima na limedumu hadi filimbi ya mwisho- akijiwekea kumbukumbu ya mwanzo mzuri Jangwani.
    Kocha Mbrazil, Marcio Maximo alipanga vikosi tofauti kila kipindi- akianza na Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Geilson Santana ‘Jaja’, Hussein Javu na Andrey Coutinho.
    Kifaa kweli; Geilson Santana 'Jaja' kulia amefungua akaunti ya mabao Jangwani leo Yanga SC ikiilaza 1-0 Chipukizi ya Pemba

    Kipindi cha pili 11 hao wote waliwapisha Juma Kaseja, Salum Telela, Edward Charles, Rajab Zahir, Said Juma, Omega Seme, Simon Msuva, Nizar Khlafan, Hamisi Kiiza, Jerry Tegete na Said Bahanuzi.
    Yanga imeweka kambi kisiwani Pemba kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo watafungua na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mabingwa Azam FC Septemba 13, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.        
    Yanga SC waliomaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita chini ya kocha Mholanzi, Hans va der Pluijm, watauanza msimu huu wa Ligi Kuu kwa mchezo na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Septemba 20, mwaka huu.
    Siku hiyo, mabingwa watetezi, Azam FC wataanza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakat washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JAJA AFUNGUA AKAUNTI YA MABAO YANGA SC IKIIADHIBU ‘KISHIKAJI’ CHIPUKIZI YA PEMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top