• HABARI MPYA

    Friday, September 19, 2014

    AZAM MEDIA WAMWAGA ‘MAHELA’ SIMBA NA YANGA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAMPUNI ya Azam Media Limited, leo imekabidhi hundi ya Sh Milioni 423.5 kwa bodi ya Ligi ya Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa ajili ya haki za matangazo ya Telesheni ya ligi hiyo.
    Fedha zitagawiwa kwa klabu 14 za Ligi Kuu, Azam FC, Simba SC, Yanga SC, Mtibwa Sugar, Kagera Sugar, Ndanda FC, Polisi Morogoro, Coastal Union, Mgambo JKT, Stand United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mbeya City na Prisons kila kilabu ikipata Sh. Milioni 27.5, hiyo ikiwa ni awamu ya pili ya mgawo wa Sh. Milioni 110 za msimu.
    Akikabidhi fedha hizo, jingo la Golden Jubilee, Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Muingereza Rhys Torrington alisema kwamba fedha zitakuwa zinatoka kwa awamu nne, na awamu mbili zilizobaki zitatolewa mzunguko wa pili wa ligi hiyo mwakani.
    Ziwafikie Simba, Yanga na wote; Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited, Rhys Torrington kushoto akimkabidhi hundi ya fedha hizo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Silas Mwakibinga leo
    “Nia ya Azam Media Limited kudhamini Ligi Kuu ni kutaka iwe na ushindani ambao utaleta mvuto na iwe nzuri zaidi miongoni mwa ligi za Afrika Mashariki,”amesema. Ameongeza kwamba sasa Azam Media Limited imetanua wigo wa huduma zake na inaonekana karibu nchi zote za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni imani yao Ligi Kuu itatangazika zaidi kimataifa.
    Akizungumzia mechi za ufunguzi za ligi hiyo wikiendi hii, Torrington amesema kwamba wataonyesha mechi tatu, ambazo ni kati ya mabingwa watetezi, Azam FC dhidi ya Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Mtibwa Sugar na Yanga SC Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Simba SC dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Ligi Kuu, Silas Mwakibinga amewashukuru Azam Media Limited kwa udhamini huo mzuri na kutekeleza vizuri Mkataba wao.
    Ametoa wito kwa marefa wa Ligi Kuu kutenda haki katika maamuzi yao ili timu bora zishinde. “Na pia kwa kupata fedha hizi mapema, naamini sasa klabu hazitakuwa na visingizio wala kelele,”amesema.
    Amesema kwamba fedha hizo zilizotolewa leo, zinafanya kila klabu hadi sasa iwe imepata Sh. Milioni 55 baada ya kupewa fungu la awali Juni 1, mwaka huu.
    Azam Media Limited waliingia Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni ya Ligi Kuu mwaka jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa pamoja na bodi ya ligi hiyo, wakitoa Sh. Milioni 100 kwa kila klabu, wakati mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 10, na kufanya dau la Milioni 110.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM MEDIA WAMWAGA ‘MAHELA’ SIMBA NA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top