• HABARI MPYA

    Sunday, September 14, 2014

    JAJA A.K.A TONI KROOS, MTAMBO MPYA WA MABAO JANGWANI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Genilson Santana Santos ‘Jaja’ leo ameongeza heshima ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Baadhi ya viongozi wa Yanga SC hawakuridhishwa na uwezo wa mchezaji huyo na wakaomba Maximo amkate, ili wasajili mchezaji mwingine watakayeona bora.
    Lakini jibu la Maximo lilikuwa ni kwamba, iwapo Jaja atakatwa naye ataondoka. Maximo akawaambia viongozi wa Yanga SC kwamba Jaja ni mtaalamu wa kufunga kama Toni Kroos wa Ujerumani na Bayern Munich. 
    Jaja akibusu Medali yake baada ya ushindi wa Ngao leo ulitokana na mabao yake mawili
    Jaja akiwa na kigogo wa Yanga SC, Seif Ahmed 'Magari' baada ya mechi
    Akasema mashabiki wakitaka kuona chenga na madoido mengine ya kisoka, wamtazame Haruna Niyonzima, lakini kwa mabao wasubiri kutoka kwa Jaja.
    Yanga SC wakawa wanaona kama Maximo anambeba Mbrazil mwenzake- lakini leo Jaja amefunga mabao muhimu katika mechi muhimu, Yanga SC ikitwaa taji la kwanza msimu wa 2014/2015.
    Jaja amefunga kipindi pili mabao mawili kabla ya Simon Msuva ‘kujazilizia’ ushindi huo kwa bao la tatu na sasa Yanga SC wanaelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu wiki ijayo kwa furaha.
    Baada ya Jaja kufunga bao la kwanza, mashabiki wa Yanga SC wakaanza kuimba jina lake- ajabu ni wale wale ambao baada ya Mbrazil huyo kumaliza dakika 45 za kwanza bila kufunga walikuwa wakimzomea.
    Mashabiki wa Yanga SC wametoka Uwanja wa Taifa wakiimba jina la Jaja na sasa wanaamini mchezaji huyo atawafunga na mahasimu wao Simba SC.
    Ukweli ni kwamba uchezaji wa Jaja ‘kivivu’ unakatisha tamaa mapema, lakini kwa kitendo cha kufunga mabao manne ndani ya mechi tano- anaweza akawa kweli mkali wa mabao kama asemavyo Maximo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JAJA A.K.A TONI KROOS, MTAMBO MPYA WA MABAO JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top