• HABARI MPYA

    Tuesday, October 21, 2014

    ALLY BUSHIRI ABWAGA MANYANGA KMKM

    Na Ameir Khalid, DAR ES SALAAM
    SINEMA kati ya kocha Ali Bushiri na uongozi wa KMKM, imefikia tamati baada ya Bushiri kutangaza rasmi kuachia ngazi, akilipiga na chini ombi la timu hiyo kumtaka arejee tena kuendelea na kibarua chake, lakini akiwa msaidizi wa Shaaban Ramadhani aliyeitwa hivi karibuni.
    Bushiri, aliyeiwezesha KMKM kutwaa ubingwa wa Zanzibar mara mbili mfululizo, katika siku za hivi karibuni aliingia kwenye sitafahamu kubwa na uongozi wa timu hiyo, baada ya kumuandikia barua ya kumsimamisha.
    Lakini, siku chache baadaye uongozi wa ‘Washika Magendo hao’ ukaamua kumrejesha Bushiri, ukimpa nafasi ya kocha msaidizi wa kocha mkuu aliyetangazwa sasa, Shaaban Ramadhani.
    Ally Bushiri amebwaga manyanga KMKM, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuonyesha kutojali thamani yake licha ya mafanikio makubwa aliyoipa timu hiyo 

    Katika mkutano na Waandishi wa Habari aliouitisha jana kwenye ukumbi wa VIP Uwanja wa Amaan, Bushiri alitaja sababu kuu mbili  zilizomfanya achukue uamuzi wa kujiuzulu.
    Kwanza alisema, hakuridhishwa na kitendo cha uongozi kumsimamisha na baadae kumtaka arejee kuwa kocha msaidizi.
    “Kwa nini mwanzo walinisimamisha bila ya sababu za msingi, na baada ya kuona timu inafanya vibaya ndio wanataka kunirejesha eti niwe kocha msaidizi,’’ alihoji.
    Bushiri alidai kwamba uongozi wa KMKM haukuwa wazi kueleza sababu za kumsimamisha, licha ya kumuandikia barua yenye maelezo ya kumtaka atoe ufafanuzi wa baadhi ya mambo baada ya kurudi na timu kutoka Kigali, Rwanda kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
    “Waliniletea barua baada ya kurudi kutoka Rwanda, lakini yote yaliyoelezwa katika barua hiyo hayana msingi. Ni vyema wangekuwa wawazi na kuueleza umma sababu hasa za kunisimamisha. Ni bora waniache niendelee na mambo yangu mengine,’’ alisisitiza.
    Bushiri, aliyewahi kuwa msaidizi kocha mkuu wa zamani wa Taifa Stars Marcio Maximo, alisema mara baada ya kupokea barua ya kurudishwa kikosini akiwa kocha msaidizi, alitoa masharti ya kuondolewa kwa kocha msaidizi Ali Vuai Shein pamoja na kocha wa makipa Salum Ali.
    Hata hivyo, alifahamisha kuwa, jambo hilo limekuwa gumu kutekelezwa na uongozi wa mabaharia hao, hivyo amewaomba radhi wapenzi wote waliokuwa wanamuunga mkono katika kipindi chake cha miaka minne ya kuifundisha timu hiyo.
    Pamoja na Bushiri kutangaza kung’atuka mbele ya waandishi wa habari, Msemaji wa KMKM Othman ‘King’ alisema bado hawajapata taarifa za hatua ya kocha huyo, kwa hivyo asingeweza  kueleza chochote hadi watakapopata barua rasmi kutoka kipa huyo zamani wa klabu za Small Simba, Malindi, na timu za taifa Zanzibar na Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALLY BUSHIRI ABWAGA MANYANGA KMKM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top