• HABARI MPYA

    Monday, October 20, 2014

    BAADA YA SIMBA NA YANGA, FIESTA NA SINEMA YA DAVIDO …SASA TUNAREJEA KWA MISS TANZANIA 2014 NA UMRI WAKE WA ANA ANA ANADOO

    JUMAMOSI iliyopita ilikuwa ya aina yake, Jumamosi ya Simba na Yanga, Jumamosi ya Fiesta, mchana masham sham na usiku masham sham.
    Tukashuhudia mechi ya watani wa jadi ikiisha kwa sare ya 0-0 lakini pia ikidhihirisha kuwa wanapokutana Simba na Yanga basi starehe kubwa ni yale majigambo ya kila pande kabla ya mchezo, kwani mara kipyenga kinapopulizwa basi kinachoonekana dimbani huwa hakina mvuto.
    Usiku wake kukawa na tamasha kubwa la muziki (Fiesta) ambalo lilihudhuriwa na umati mkubwa wa mashabiki pale Leaders Club, lakini tamasha hili kwa mara nyingine tena likaashiria kuzikwa kwa muziki wa dansi – hakuna bendi wala msanii wa dansi aliyetumbuiza kwenye Fiesta.

    Fiesta ya leo sio ile ya zamani iliyojulikana kama Summer Jam iliyokuwa ikiwapandisha jukwaani wasanii kibao wa muziki wa dansi na ikanoga kwa sana tu, siku hizi hata akibahatika kushiriki msanii wa dansi basi ni kwa nyimbo zilizokaa kibongo fleva tu.
    Lakini Fiesta hii pia ikatupatia ‘sinema’ tamu – sinema ya msanii Davido kutoka Nigeria ambaye hapo mwanzo ziliibuka habari rasmi kabisa kuwa msanii huyo amekatazwa na mahakama kupanda jukwaa la Fiesta kutokana na mgongano wa kibiashara, jamii ikaamini kuwa Davido hatapanda jukwaani lakini mwisho wa siku supastaa huyo akafanya vitu vyake Fiesta.
    Tuachane na hayo, turejee kwenye suala la mshindi wa Redds Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu ambaye tangu alipotwaa taji wiki moja iliyopita pale Mlimani City jijini Dar es Salaam, mengi yameibuka na kubwa zaidi ni umri wake, kwamba amegushi umri na eti umri wake halisi unatosha kabisa kumfanya avuliwe taji hilo kwa vile haukidhi vigezo na masharti ya kushiriki Miss Tanzania.
    Umri halisi wa Sitti unachanganya sana, hususan unapopitia habari za mitandao kadhaa ya kijamii – ipo inayosema ana umri wa miaka 18, mingine ikisema 25, ipo hata iliyokwenda mbali zaidi na kusema ana umri wa miaka 29. 
    Kwa mfano ukibofya link hii hapa http://ujijirahaa.blogspot.com/2014/06/patashika-miss-changombe-2014.html, utakutana na habari ya fainali za Miss Chang’ombe 2014 huku umri wa Sitti ukitajwa kuwa ni miaka 22, lakini mmoja wa mabosi wa kamati ya Miss Tanzania Bosco Majaaliwa yeye alinukuliwa hivi karibuni akisema Sitti ana umri wa miaka 23.
    Hati za kusafiria pamoja na leseni ya kuendeshea gari zinaonyesha kuwa Sitti ana umri wa miaka 25, kama nyaraka hizo zilizowekwa mtandaoni ni za kweli au si kweli, ni yeye mwenyewe ndiye wa kutujuza.
    Nimebahatika kutazama fainali zote za Miss Tanzania kuanzia ile ya kwanza ya mwaka 1994 aliyoshinda Aina Maeda, lakini kwa bahati mbaya kinyang’anyiro cha Miss Tanzania 2014, kilinipitia kushoto, hivyo sikubahatika kusikiliza kwa masikio yangu ni umri gani aliojitambulisha nao Sitti jukwaani.
    Kamati ya Miss Tanzania itafanya mkutano na waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki hii, wengi tunataraji kuwa tutapata mwanga juu ya umri halisi wa Sitti ikiwa ni pamoja na kusafishwa kwa ukungu wote uliotanda juu yake likiwemo la madai ya kuwa tayari ana mtoto, madai ya rushwa na hata mbegu mbaya za ushabiki wa kisiasa zinazopandikizwa.
    Sifa za kwanza za mtu anayepaswa kushiriki Miss Tanzania na hatimaye Miss World ni kuwa na umri kati ya miaka 18 na 24, asiwe amezaa wala asiwe ameolewa.
    Kwa mtazamo wangu hadi mshindi anapatikana, sina cha kuilaumu kamati ya Miss Tanzania, hususan katika suala la umri - nimeambiwa safari hii washiriki waliwasilisha vyeti vya kuzaliwa, Kamati ya Miss Tanzania ingehitaji nini tena zaidi ya hilo? Hakuna.
    Sehemu ndogo ninayowalaumu waandaji kuanzia ngazi za vitongoji hadi fainali ya Miss Tanzania ni kushindwa kubaini uwiano wa umri na usomi wa Sitti – iwe ni miaka 18 au 23, bado umri wake hauwiani hata kidogo na jumla ya miaka aliyotumia kwenye kusaka elimu
    Jambo moja liko wazi: Kama nyaraka zilizosambaa mitandaoni ni ya kweli, basi Sitti atakuwa amegushi moja ya nyaraka zake muhimu – kama si cheti cha kuzaliwa basi ni hati ya kusafiria pamoja na leseni ya kuendeshea gari. Ni vema Sitti akachukua hatua haraka na kuuleza umma ni kipi alichogushi, kwa dhamira ipi? Kwa malengo yepi?  Hadi Jumatatu ijayo, sina la ziada.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAADA YA SIMBA NA YANGA, FIESTA NA SINEMA YA DAVIDO …SASA TUNAREJEA KWA MISS TANZANIA 2014 NA UMRI WAKE WA ANA ANA ANADOO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top