• HABARI MPYA

    Thursday, October 23, 2014

    CANNAVARO, AGGREY MORRIS NA MWADINI WAREJESHWA ZANZIBAR HEROES KWA AJILI YA CHALLENGE

    Na Ameir Khalid, ZANZIBAR
    WACHEZAJI Nadir Haroub 'Cannavaro', Aggrey Morris na mlinda mlango Mwadini Ali, wamerejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ya soka Zanzibar, 'The Zanzibar Heroes'.
    Akitangaza wachezaji watakafanya mazoezi kwa ajili ya kupata kikosi kitakachoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu yatakayofanyika nchini Ethiopia, kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema amewateua wanandinga hao na wengine waliotemwa mwaka jana ili kurejesha mshikamano.
    Kwa ujumla, Morocco ametangaza wachezaji 36 ambao watafanya mazoezi na baadae kuchuja ili kupata 20 wa mwisho watakaopeperusha bendera ya Zanzibar kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
    Hata hivyo, alisema haikuwa kazi rahisi kufanya uteuzi huo, na alilazimika kufanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Tanzania Bara ili kuangalia na kujiridhisha na viwango vya wachezaji  hao.
    Aggrey Morris kulia amerejeshwa kikosini Zanzibar Heroes 

    Alisema kigezo chengine alichozingatia, ni iwapo wachezaji hao wanapata nafasi ya kuzichezea klabu zao kwenye mechi za ligi na nyengine.
    Wachezaji hao na timu wanazotoka kwenye mabano, ni makipa; Mwadini Ali (Azam), Khalid Mahadhi (Mafunzo), Mudathir Yahya (KMKM) na Mwalimu Ali (Prisons).
    Mabeki; Mohammed Othman (Polisi), Said Mussa (Mafunzo), Shafii Hassan (Zimamoto), Ismail Khamis (JKU), Adeyoum Saleh (Chuoni), Edward Peter (Hard Rock), Nadir Haroub 'Cannavaro' (Yanga SC), Nahoda Bakari( Polisi Moro), Aggrey Morris na Abdallah Sebo (Azam), Nassor Masoud ‘Chollo’ na Abdulaziz Makame (Simba SC), Mohammed Faki ( JKT Ruvu) na Khamis Ali (KMKM).
    Viungo ni Mohammed Issa (Chuoni), Mohammed Abdulrahim, Ali Juma (Mafunzo), Amour Suleiman (Malindi), Makame Hamad (Zimamoto), Awadh Juma (Simba), Khamis Mcha 'Vialli', Mudathir Yahya (Azam), Abdulhalim Humoud (Sofapaka-Kenya) na Suleiman Kassim 'Selembe' (Polisi Moro).
    Washambuliaji; Omar Juma (Hard Rock), Mohammed Seif (Dogomoro), Fasihi Hija (Malindi), Simai Masoud (Fufuni), Nyange Othman, Ibrahim Hilika (Zimamoto), Said Juma ‘Kizota’ (Yanga) na Ame Ali (Mtibwa Sugar).
    Kocha huyo ametaja mikakati ya mazoezi kwamba ameigawa katika sehemu mbili, akianza na wachezaji waliopo Zanzibar na baadaye atajumuisha walioko nje ya Zanzibar wakati ligi zitakaposimama.
    Alifahamisha kuwa, awali alipanga kuanza mazoezi mwezi huu wa Oktoba, lakini hilo limeshindikana na badala yake itakuwa Novemba mosi.
    Morocco alieleza kuwa tayari amekiagiza Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kujaribu kutafuta mechi za kirafiki ili kujipima nguvu.
    Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA Masoud Attai, alisema kuwa, tayari wameshatuma barua nchi za Kenya na Uganda kupitia vyama vyao vya soka kuomba mechi hizo na kinachisubiriwa ni majibu.
    Attai amewaomba wafanyabiashara mbalimbali kujitokeza kuisadia timu hiyo, ili iweze kujiandaa vyema kwani inahitaji fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CANNAVARO, AGGREY MORRIS NA MWADINI WAREJESHWA ZANZIBAR HEROES KWA AJILI YA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top