• HABARI MPYA

    Monday, October 20, 2014

    CHOVE: TUTAWASIMAMISHA AZAM FC, JKT IKO BOMBA MBAYA SASA HIVI

    Na Mahmoud Zubeiry, MBEYA
    KIPA namba moja wa JKT Ruvu, Jackson Chove amesema kwamba wataisimamisha Azam FC mwishoni mwa wiki watakapokutana nayo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Sokoine, Mbeya- kipa huyo wa zamani wa Yanga na Coastal Union, amesema kwamba wana matumaini ya kuifunga Azam FC Jumamosi.
    “Siku Azam wanacheza na Mbeya City (Sokoine) sisi tulikuwa jukwaani tunawatazama. Wanafungika. Na tutawafunga wale nakuambia,”amesema Chove. 
    Jackson Chove amesema Azam FC wanafungika 

    Hata hivyo, Chove aliyewahi pia kucheza soka ya kulipwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Rwanda, amesema pamoja na dhamira ya kushinda, mchezo huo utakuwa mgumu.
    Akifafanua amesema; “Tulikuja kuona mechi yao na Mbeya City ili tuwajue wanachezaje, ni timu nzuri kwa kweli, ila kwa tulivyoiona tunaweza kuifunga. Na kwa sasa timu yetu ipo vizuri sana,”amesema Chove.
    Chove aliiongoza JKT Ruvu kupata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu jana baada ya kuifunga Prisons 2-1 Uwanja wa Sokoine.
    Matokeo hayo, yanaifanya JKT sasa iwe na pointi nne, ambazo zote imevuna Uwanja wa Sokoine, baada ya Septemba 21, kutoka sare ya bila kufungana na Mbeya City, wakati mechi nyingine ilifungwa Dar es Salaam 2-0 na Kagera Sugar na 2-1 na Yanga SC.
    Katika mchezo wa jana uliochezeshwa na refa Mary Kapinga wa Ruvuma, aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Joseph Pombe wa Shinyanga, timu hizo zilikwenda kupumzika zikiwa tayari zimekwishafungana bao 1-1.
    JKT Ruvu inayofundishwa na Freddy Felix Minziro, ilikuwa ya kwanza kupata bao, lililofungwa na Najim Magulu dakika ya 27 baada ya pasi nzuri ya Jabir Aziz na kumtoka beki wa Prisons kabla ya kumchambua kipa Beno Kakolanya.
    Prisons ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Amir Omar dakika ya 35 aliyemalizia krosi ya Jacob Mwaitakalo akitumia mwanya wa mabeki wa JKT kuchanganyana na kipa wao, Jackson Chove.
    Kipindi cha pili, JKT Ruvu walikianza vizuri wakicheza kwa na kasi za pasi ndefu- jambo ambalo liliwafanya wapate bao la ushindi mapema.
    Alikuwa ni kiungo wa zamani wa Simba SC na Azam FC, Jabir Aziz Stima aliyeifuyngia timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa bao la ushindi dakika ya 
    51 kwa penalti baada ya kipa Beno Kakolanya kumchezea rafu mshambuliaji Iddi Mbaga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHOVE: TUTAWASIMAMISHA AZAM FC, JKT IKO BOMBA MBAYA SASA HIVI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top