• HABARI MPYA

    Sunday, October 19, 2014

    JABIR AZIZ AING’ARISHA JKT RUVU MBEYA, YAICHAPA PRISONS 2-1 SOKOINE LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, MBEYA
    JKT Ruvu imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, baada ya kuilaza Prisons mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Matokeo hayo, yanaifanya JKT sasa iwe na timu nne, ambazo zote imevuna Uwanja wa Sokoine, baada ya Septemba 21, kutoka sare ya bila kufungana na Mbeya City, wakati mechi nyingine ilifungwa Dar es Salaam 2-0 na Kagera Sugar na 2-1 na Yanga SC.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mary Kapinga wa Ruvuma, aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Joseph Pombe wa Shinyanga, timu hizo zilikwenda kupumzika zikiwa tayari zimekwishafungana bao 1-1.
    Pati la ushindi; Wafungaji wa mabao ya JKT dhidi ya Prisons, Jabir Aziz kulia na Najim Magulu katikati wakipongezana kwa pamoja na Iddi Mbaga kushoto

    JKT Ruvu inayofundishwa na Freddy Felix Minziro, ilikuwa ya kwanza kupata bao, lililofungwa na Najim Magulu dakika ya 27 baada ya pasi nzuri ya Jabir Aziz na kumtoka beki wa Prisons kabla ya kumchambua kipa Beno Kakolanya.
    Prisons ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Amir Omar dakika ya 35 aliyemalizia krosi ya Jacob Mwaitakalo akitumia mwanya wa mabeki wa JKT kuchanganyana na kipa wao, Jackson Chove.
    Kipindi cha pili, JKT Ruvu walikianza vizuri wakicheza kwa na kasi za pasi ndefu- jambo ambalo liliwafanya wapate bao la ushindi mapema.
    Alikuwa ni kiungo wa zamani wa Simba SC na Azam FC, Jabir Aziz Stima aliyeifuyngia timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa bao la ushindi dakika ya 
    51 kwa penalti baada ya kipa Beno Kakolanya kumchezea rafu mshambuliaji Iddi Mbaga.
    Baada ya bao hilo, JKT walianza kucheza kwa kujihami huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza na tangu hapo, kipa wao Jackson Chove ‘Mandanda’ alianguka mara mbili akivua glavu na kutupa kabisa.
    Wachezaji watatu wa ndani wa JKT nao walikuwa wakianguka pia na kupatiwa huduma ya kwanza.
    Dakika ya 87 Nurdin Chona aliyetokea benchi alikosa bao la wazi baada ya shuti lake akiwa ndani ya sita kupaa juu ya lango akiwa amebaki yeye na kipa, kufuatia pasi ya Amir Omar.
    Matokeo hayo yanawafanya wana Mbeya wazidi kuwa wanyonge juu ya timu zao, baada ya jana pia Mbeya City kufungwa 1-0 na Azam FC. 
    Kikosi cha Prisons kilikuwa; Beno Kakolanya, Boniface Hau, Nurdin Chona, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhil, Hamisi Maingo/Julius Kwanga dk80, Freddy Chudu, Jacob Mwaitalako/John Matei dk52, Amir Omar na Jeremiah Juma.
    JKT Ruvu; Jackson Chove, Ramadhani Shamte, Nafo Zuberi, Ramadhani Madenge, Renatus Morris, George Minja, Damas Makwaya/Amos Mgisa dk46, Jabir Aziz, Iddi Mbaga, Najim Magulu/Alex Abel dk79 na Ally Bilal/Nashon Naftali dk86.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JABIR AZIZ AING’ARISHA JKT RUVU MBEYA, YAICHAPA PRISONS 2-1 SOKOINE LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top