• HABARI MPYA

    Thursday, October 23, 2014

    JAMES KENNEDY MWAISABULA: KIPA WA PRISONS ‘YANGA DAMU’ MWENYE NDOTO ZA KUWA ‘TANZANIA ONE’

    Na Saada Salim, MBEYA 
    HAKUNA mwanadamu ajuaye siku yake inayofuata, hii ni kauli ya kipa chipukizi wa kikosi cha timu ya vijana ya Tanzania Prisons ya Mbeya, James Kennedy Mwasabula, aliyekuwa na ndoto ya kuwa Mhandisi wa magari baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari, lakini akaangukia kwenye soka.
    Licha ya baba yake Kennedy Mwaisabula kujihusisha na mambo ya soka, lakini James hakuwa na ndoto za moja kwa moja kuwa mchezaji kama ilivyo kwa sasa kutuliza akili yake katika soka.
    BIN ZUBEIRY lilifanya mahojiano na kinda huyo kwa kueleza mambo mbalimbali kuhusu maisha yake, malengo pamoja na kile kilichopelekea kutotimiza malengo yake.
    Kinda huyo aliyezaliwa mwaka 1993 Kibaha mkoani Pwani, elimu yake ya msingi aliipatia katika shule ya Mchikichini, Ilala mjini Dar es Salaam, ambapo alibahatika kuchanguliwa Sekondari Pwani.
    James Kennedy Mwaisabula akiwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kabla ya Prisons kucheza na JKT Ruvu mwishoni mwa wiki

    KUTOTIMIZA NDOTO YAKE:
    James anasema katika akili yake kitu cha kwanza alifikiria kuja kusoma kwa juhudi aje kuwa Mhandisi wa magari, ambapo baada ya kupata matokeo mabaya ya kidato cha Nne ndoto zake zimefutika na amegeukia soka.
    “Kipaji cha soka ninacho, lakini hapo awali sikuweka akilini sana, kwani akili yangu kuwa Mhandisi wa magari, baada ya matokeo mabaya ya kidato cha Nne ndoto hizo zimefutika sasa na kutulia katika soka,” anasema.

    SABABU YA KUCHEZA PRISONS:
    James anasema anaamini kuna timu nying hapa nchini angeweza kucheza katika vikosi vya timu za vijana, lakini baada ya kuhitimu mafunzo yake ya uaskari katika jeshi la Magereza, akuchukuliwa na timu hiyo moja kwa moja.
    “Kwa sasa ni mwajiriwa wa Magereza, nimepata nafasi ya kucheza hapa baada ya kumaliza mafunzo yangu ya uaskari Magereza katika chuo cha Kiwila, Tukuyu (Mbeya),”anasema.
    James anasema baada ya kumaliza mafunzo hayo. Kocha Msaidizi wa Prisons, Shaaban Kazumba alimfuata na kumuomba ajiunge na timu ya vijana ya klabu hiyo ya Ligi Kuu, wakati huo akiwa anacheza katika timu ya mtaani ya Black Tiger.

    MALENGO YAKE:
    Wachezaji wengi chipukizi Afrika unapowauliza juu ya malengo yake ya baadaye, watakuambia ni kueleza kucheza ulaya, lakini kwa James kwake ni tofauti, kwani anafikiria zaidi kutaka kusaidia taifa lake.
    “Huwa nawaza kujituma na siku moja ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa, Stars kwani natamani siku moja nije kuipeperusha vyema bendera ya taifa langu katika michuano ya kimataifa. Nataka kuwa kipa namba moja wa Taifa Stars,” anasema kinda huyo.
    Kuhusu kuchezea timu kubwa, kati ya Yanga, Simba na Azam, mtoto huyo wa kocha na mchambuzi maaurufu wa soka nchini, Kennedy Mwaisabula, anasema hiyo ipo akilini mwake. “Malengo hayo nayafikiria sana, napenda siku moja nije kuchezea Yanga, kwani ni timu niipendayo tangu nikiwa mdogo,”anasema.
    James anasema anamshukuru sana baba yake ambaye enzi zake naye alicheza soka, kwa sapoti kubwa aliyompa hadi kufika hapa na anaamini ipo siku atatimiza ndoto zake.
    Kipa huyo mwenye umbo kubwa aliyejengeka kimichezo haswa, anasema atajibidiisha kwa mazoezi hadi afanikiwe kutimiza malengo hayo. Naam, huyo ndiye James Kennedy Mwaisabula kipa wa Prisons mwenye mapenzi na Yanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JAMES KENNEDY MWAISABULA: KIPA WA PRISONS ‘YANGA DAMU’ MWENYE NDOTO ZA KUWA ‘TANZANIA ONE’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top