• HABARI MPYA

    Monday, October 20, 2014

    PETER MANYIKA AWEKA REKODI MBILI NZITO SIMBA SC HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU...

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIPA mwenye umri wa miaka 19, Peter Manyika Jumamosi aliweka rekodi mbili- kwanza ya kuwa kipa wa kwanza kuidakia klabu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanania Bara msimu huu bila kufungwa.
    Lakini rekodi ‘babu kubwa’ ni kuwa kipa wa kwanza wa Simba SC kudaka dhidi ya mahasimu bila kufungwa tangu Mei 6, mwaka 2012.
    Katika msimu huu, Simba SC imecheza mechi nne na kutoa sare zote, 2-2 na Coastal Union na 1-1 mara mbili na Stand United na Polisi Morogoro.
    Sare ya 2-2 langoni alikuwa Ivo Mapunda na zilizofuata, alikuwa Hussein Sharrif ‘Casillas’.
    Peter Manyika ameweka rekodi mbili Simba SC

    Lakini kuelekea mechi na Yanga SC, makipa wote hao, Ivo namba moja na Casillas namba mbili wakawa majeruhi, hivyo dogo Manyika akasimamishwa langoni na kumaliza dakika 90 bila kufungwa timu hizo zikitoka sare ya 0-0.
    Juma Kaseja alikuwa kipa wa mwisho kuidakia Simba dhidi ya Yanga bila kufungwa Mei 6, mwaka 2012 Wekundu wa Msimbazi wakiwafunga watani wao hao wa jadi mabao 5-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
    Tangu ushindi huo uliotokana na mabao ya Emmanuel Okwi mawili dakika ya pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti pia dakika ya 67 na Patrick Mafisango (marehemu) kwa penalti dakika ya 72, timu hizo zimekutana mara nne sita katika mashindano yote.
    Oktoba 3, 2013 zilitoka sare ya 1-1, Amri Kiemba akitangulia kuifungia Simba SC dakika ya tatu, kabla ya Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga SC kwa penalti dakika ya 65, langoni akiwa Kaseja.
    Mei 18, mwaka 2013,  Yanga ilishinda mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Didier Kavumbangu dakika ya tano na Hamisi Kiiza dakika ya 62 langoni akiwa Kaseja.
    Oktoba 20, mwaka 2013 timu hizo zilitoka sare ya 3-3, Yanga wakitangulia kufunga kipindi cha kwanza mabao ya Mrisho Ngassa dakika ya 15 na Hamisi Kiiza dakika ya 36 na 45, langoni akiwa Abel Dhaira kabla ya Simba SC kusawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Betram Mombeki dakika ya 54, Joseph Owino dakika ya 58 na Gilbert Kaze dakika ya 85.
    Desemba 21, mwaka 2013 Simba SC iliifunga 3-1 Yanga katika mechi ya Nani Mtani Jembe, mabao ya Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44 kwa penalti na Awadh Juma wakati bao la kufutia machozi la watani wao lilifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 87, langoni akiwa Ivo Mapunda.  
    Aprili 19, mwaka 2014 timu hizo zilitoka sare ya 1-1, Haroun Chanongo akitangulia kuifungia Simba SC dakika ya 76 kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga SC dakika ya 86, langoni akiwa Ivo Mapunda.
    Lakini Jumamosi, Oktoba 18, 2014 mtoto wa kipa wa zamani wa Yanga SC, Manyika Peter alidaka dakika 90 na ushei bila kufungwa katika sare ya 0-0.  Je, huyu ni shujaa mpya wa langoni Simba SC? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PETER MANYIKA AWEKA REKODI MBILI NZITO SIMBA SC HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top