• HABARI MPYA

    Sunday, October 19, 2014

    SIMBA SC WAINGIA MKATABA NA JOMO SONO, TIMU KUWEKA TENA KAMBI AFRIKA KUSINI DESEMBA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeingia Mkataba na Jomo Sono, mmiliki wa klabu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini kuitafutia kambi ya maandalizi nchini humo timu yake kwa mwezi wote wa Desemba.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, kikosi cha timu hiyo kitakwenda Afrika Kusini tena mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa kambi ya mwezi mmoja.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kwamba wameingia Mkataba na Sono maarufu kama Black Prince aitafutie Simba SC kambi nzuri ya mazoezi pamoja na kuandaa mechi za kujipima nguvu.
    Mipango; Zacharia Hans Poppe kulia akiwa na kocha wa Simba SC, Patrick Phiri nchini Afrika Kusini hivi karibuni

    Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuiandaa timu kwa ajili ya mechi za mwisho za mzunguko wa kwanza na mzunguko mzima wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Poppe amesema kwamba kwa sasa wamewekeza zaidi katika kujenga timu ambayo itarejesha utawala wa Simba SC katika ya Tanzania baadaye.
    “Hatujafungwa hata mechi moja kwa sasa (katika Ligi Kuu), lakini hatujashinda pia. Hicho si kitu kizuri na si kwa sababu timu yetu ni mbaya, hapana, bali tunakosa bahati tu,”.
    “Ila naamini kila jambo lenye mwanzo halikosi mwisho wake, naamini baada ya sare hizi nne, sasa wakati wa Simba SC kushinda umewadia, na tukianza kushinda, wimbi la ushindi litaendelea hadi mwisho,”amesema.
    Poppe amesema dira ya uongozi wa klabu yao chini ya Rais, Evans Aveva inaangalia miaka mitano ijayo Simba SC itakuwaje, ndiyo maana hata aina ya usajili wao umezingatia hilo.
    “Tumesajili chipukizi wengi, ambao wengi wao tumewatoa timu yetu ya vijana, ili wapate uzoefu na kucheza kwa muda mrefu. Bila shaka watu wameona ubora wa vijana hawa wadogo hadi sasa,”amesema.
    Simba SC iliweka kambi ya wiki na ushei Afrika Kusini kabla ya mechi na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Jumamosi iliyoisha kwa sare ya bila kufungana.
    Wekundu hao wa Msimbazi wametoa sare mechi zao zote nne za mwanzo za Ligi Kuu, 2-2 na Coastal Union na 1-1 mara mbili na Polisi Moro na Stand United kabla ya kutoka 0-0 na Yanga, mechi zote ikicheza Uwanja wa nyumbani, Taifa mjini Dar es Salaam.
    Simba SC inatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza ya ugenini mwishoni mwa wiki ijayo, itakapokuwa mgeni wa Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAINGIA MKATABA NA JOMO SONO, TIMU KUWEKA TENA KAMBI AFRIKA KUSINI DESEMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top