• HABARI MPYA

    Wednesday, October 22, 2014

    SIMBA SC YAINGIA KATIKA WAKATI MWINGINE MGUMU ZAIDI LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BAADA ya mechi nne mfululizo za nyumbani katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC itacheza mechi yake ya kwanza ugenini mwishoni mwa wiki.
    Simba SC itacheza na Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi, Ikitoka kutoa sare nne katika mechi zote za mwanzo, 2-2 na Coastal Union, 1-1 na Polisi Moro, 1-1 na Stand Unted na 0-0 na Yanga SC.
    Katika Ligi yetu, nyumbani ni sehemu nzuri ya kuvuna pointi kuliko ugenini, hususan timu za Dar es Salaam zinaposafiri mikoani na kwenda kukutana na viwanja vyenye hali isiyo nzuri sana katika eneo la kuchezea.
    Jonas Mkude alitoka dakika ya 60 baada ya kuumia dhidi ya Yanga SC na kipa Peter Manyika ataendelea kudaka mwenyewe wakati kaka zake, Ivo Mapunda na Hussein Sharrif 'Casillas' wakiwa majeruhi  

    Sasa Simba SC ndiyo wanaingia katika wakati huo, kwani baada ya mechi na Prisons Jumamosi, wiki inayofuata watakuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kumenyana na Mtibwa Sugar Novemba 1, kabla ya kurejea tena Dar es Salaam kucheza na Ruvu Shooting Novemba 9.
    Huo utakuwa mchezo wa mwisho kabla ya mapumziko marefu ya karibu mwezi mzima kupisha Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge na michuano ya vijana ya Kombe la Uhai, inayohusisha klabu za Ligi Kuu hadi Desemba 26 ligi hiyo itakaporejea tena.   
    Simba SC haijashinda mechi kati ya nne ilizocheza nyumbani na katika mechi zake tatu zijazo, mbili itacheza ugenini tena dhidi ya timu ambazo zinapokuwa nyumbani kwao, hushinda mara nyingi.
    Tayari kuna shinikizo la mashabiki kutaka timu ishinde baada ya sare hizo nne za nyumbani- na bahati mbaya Simba SC inakwenda kwenye mchezo mgumu zaidi.
    Kipa Ivo Mapunda bado hajapona na anahitaji wiki mbili zaidi kabla ya kuanza mazoezi taratibu, Hussein Sharrif ‘Casillas’ naye si wa kumtarajia mwaka huu kucheza- maana yake klabu itacheza mechi hizo ikiwa na kipa mmoja tu, Peter Manyika.
    Wachezaji wa Simba SC watakuwa na mechi mbili mfululizo za ugenini kuanzia wikiendi hii

    Huyo ni wa kumuombea naye asiumie na wala asipate adhabu ya kumzuia kucheza- wakati huo huo wachezaji wengine majeruhi akina Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Miraj Adam, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Kiongera, Jonas Mkude na Amisi Tambwe mustakabali wao bado haueleweki.
    Wazi mashabiki wa Simba SC wanatakiwa kushikamana sana na timu yao kwa wakati huu mgumu, wakijua hali halisi kwamba wapo katika kipindi kigumu cha mpito.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAINGIA KATIKA WAKATI MWINGINE MGUMU ZAIDI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top