• HABARI MPYA

    Friday, October 24, 2014

    YANGA SC WAPATA MAPOKEZI YA MAANA SHINYANGA

    Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
    KIKOSI cha Yanga SC kimewasili mjini Shinyanga mchana wa leo na kupata mapokezi makubwa tayari kwa mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya wenyeji, Stand United.
    Yanga SC imewasili mjini humo salama, ikitokea Dodoma ambako ilisimama kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya CDA ya Dodoma jana.
    Mashabiki wa Yanga SC walianza kulishangilia basi la timu hiyo mara baada ya kuliona tu likiingia mjini Shinyanga kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Mashabiki waliojitokeza kuipokea Yanga SC ikiwasili Shinyanga leo

    Yanga SC jana ililazimishwa sare ya bila kufungana na CDA ya Dodoma katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Kocha Mbrazil, Marcio Maximo jana aliwaanzisha wachezaji wake wa akiba, ambao walishindwa kufurukuta mbele ya timu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili.
    Shambulizi la maana ambalo Yanga SC walifanya kipindi cha kwanza ilikuwa dakika ya 40, baada ya Mganda Hamisi Kiiza kupata krosi nzuri na kumpa pasi nzuri pia Jerry Tegete ambaye katika mastaajabu ya wengi, akapiga nje.
    Na kipindi cha pili, Said Bahanuzi naye alipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 85 baada ya kuunganishia nje kwa shuti kubwa krosi ya Salum Telela.
    Wachezaji waliocheza jana ni Juma Kaseja ambaye alimpisha Ally Mustafa ‘Barthez’, Salum Telela, Amos Abel, Patrick Ngonyani, Rajab Zahir, Said Juma ‘Kizota’, Omega Seme, Nizar Khalfan, Hussein Javu, Jerry Tegete na Hamisi Kiiza aliyempisha Said Bahanuzi.
    Hadi sasa, Yanga SC ina pointi saba katika Ligi Kuu ilizovuna katika mechi nne za awali, baada ya kufungwa 2-0 Mtibwa Sugar mjini Morogoro na kushinda 2-1 mara mbili mfululizo dhidi ya Prisons na JKT Ruvu, kabla ya sare ya 0-0 na mahasimu wao, Simba SC. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAPATA MAPOKEZI YA MAANA SHINYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top