• HABARI MPYA

    Tuesday, November 18, 2014

    KIPRE TCHETCHE APIGWA BEI AZAM FC, TRAORE AJA KUZIBA NAFASI YAKE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    AZAM FC inasubiri kupokea majibu ya ofa kutoka klabu ya Kelntan FC ya Malaysia, ili kumuuza mshambuliaji wake Kipre Herman Tchetche raia wa Ivory Coast, wakati huo huo iko katika mpango wa kumchukua mshambuliaji kutoka Mali, Mohamed Traore.
    “Ndiyo, kuna ofa kutoka Kelantan FC, imefika Azam FC na wanaendelea na majadiliano, nasubiri kusikia kutoka kwao, nipo tayari kwa lolote (kubaki, au kuondoka). Mimi ni mchezaji, naweza kucheza popote,”amesema Kipre Tchetche akizungumza na BIN ZUBEIRY leo.
    Tayari Azam FC wamefikia hatua nzuri katika kumsajili mchezaji mwingine wa El Merreikh ya Sudan, Mohamed Traore baada ya kumpata mchezaji mwingine kutoka klabu hiyo, Serge Wawa Pascal.
    Kipre Tchetche yuko mbioni kuondoka Azam FC baada ya miaka minne ya mafanikio, akishinda nayo mataji manne

    Wiki iliyopita Azam FC iliingia Mkataba na beki wa kati, Serge Wawa raia wa Ivory Coast na sasa inaharakisha mpango wa kumchukua mshambuliaji Traore, ili azibe pengo la Kipre aliye mbioni kuuzwa.
    Traore maarufu kama ‘Zorro wa Bamako’, mwenye umri wa miaka 26 sasa na urefu wa futi 6, ni mshambuliaji mwenye uzoefu mkubwa baada ya kuchezea klabu kadhaa kubwa barani Afrika.
    AS Real Bamako ya Bamako, kwao Mali ndiyo iliyomuibua mwaka 2007 kabla ya kununuliwa na Club Africain ya Tunisia mwaka 2009, baadaye Al-Nasr Benghazi ya Libya 2011, FC Sion mwaka huo huo, Ismailia ya Misri 2010 Al-Hilal Omdurman ya Sudan 2013 kabla ya mwaka huu kutua Merreikh. 
    Kipre mwenye umri wa miaka 27 sasa, mchezaji wa zamani wa timu za vijana za Ivory Coast kuanzia chini ya umri wa miaka 17, U20 na U23, alijiunga na Azam FC mwaka 2011 akitokea JC Abidjan ya nyumbani kwao.
    KIfaa kinakuja; Mohamed Traore anakuja kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche Azam FC

    Katika kipindi hicho, mshambuliaji huyo hatari ameisaidia klabu hiyo kushinda mataji manne, Kombe la Mapinduzi mara mbili 2012 na 2013, Kombe la Hisani DRC 2012 na Ligi Kuu msimu uliopita.
    Pia amekuwa Mfungaji wa Ligi Kuu msimu wa 2012/2013 na katika kipindi chote hicho amekuwa tegemeo la mabao katika klabu ya Azam FC. Vigogo wa soka Tanzania, Yanga SC wamekuwa wakisotea saini ya mchezaji huyo kwa misimu miwili iliyopita bila mafanikio.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPRE TCHETCHE APIGWA BEI AZAM FC, TRAORE AJA KUZIBA NAFASI YAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top