• HABARI MPYA

    Tuesday, November 18, 2014

    MAXIMO AREJEA DAR KUISUKA UPYA YANGA SC, ATAKA MAMBO MATATU ILI TIMU IWE TISHIO

    Na Abdul Salim, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo anatarajiwa kurejea mwishoni mwa wiki na timu yake nzima, Msaidizi wake Leonardo Leiva na wachezaji Andrey Coutinho na Genilson Santana Santos ‘Jaja’.
    Maximo na Wabrazil wenzake hao wanaofanya naye kazi Yanga SC, walikwenda kwao kwa mapumziko mafupi kufuatia kusimama kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wiki iliyopita.
    Na atakaporejea, Maximo kuanza maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu itakayorejea mwezi ujao mwishoni, anatarajiwa kukumbushia maagizo matatu aliyowaachia viongozi wa Yanga SC ili afanye kazi yake vizuri.
    BIN ZUBEIRY inafahamu, kabla ya kuondoka Maximo aliomba Uwanja wa Kaunda ukarabatiwe ili timu iwe inafanyia mazoezi hapo, kwa sababu kwa sasa anashindwa kutekeleza programu zake vizuri kutokana na kutumia viwanja vya kukodi.
    Kocha wa Yanga SC, Marcio Maximo anatarajiwa kurejea mwishoni mwa wiki na kukumbushia mambo matatu aliyowaagiza viongozi wa klabu 

    Maximo aliwaambia viongozi wa Yanga SC anahitaji kufanya mazoezi kwa siku mara mbili, lakini kwa kutumia viwanja vya kukodi anashindwa kutekeleza hilo, kutokana na ugumu wa kuwakusanya wachezaji wanaoishi sehemu tofauti mara mbili siku.
    Aidha, Maximo pia alilalamikia ukosefu wa vifaa vya kutosha vya mazoezi pamoja na upungufu hata wa vitendea kazi na dawa kwa ajili ya wachezaji wanapokuwa wagonjwa au majeruhi.
    Jambo la tatu, ambalo Maximo alilalamikia ni suala la maslahi ya wachezaji wake, kwamba kuna baadhi ya wachezaji wana madai ya fedha ambazo uongozi umeshindwa kuyalipa kwa wakati, hivyo kuwafanya wapoteze ufanisi kazini.
    Tegemeo la mabao la Yanga SC, Genilson Santana Santos 'Jaja' naye atawasili mwishoni mwa wiki

    Maximo anaamini kama wachezaji wake hawatakuwa vizuri kifikra hawawezi kufanya kazi vizuri, hivyo wakati anaondoka aliuagiza uongozi uyashughulikie masuala hayo.
    Na wakati Mbrazil huyo anatarajiwa kurejea mwishoni mwa wiki- ni matarajio kwamba uongozi wa klabu chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji utakuwa umeyafanyia kazi yote hayo. 
    Maximo alianza kazi Yanga SC Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijim ambaye aliondoka baada ya msimu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO AREJEA DAR KUISUKA UPYA YANGA SC, ATAKA MAMBO MATATU ILI TIMU IWE TISHIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top