• HABARI MPYA

    Saturday, December 20, 2014

    MKUTANO MKUU TFF MACHI 14 SINGIDA, MATUMIZI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepanga Mkutano Mkuu wa Kawaida wa mwaka ufanyike Machi 14 na 15 mwakani mjini Singida.
    Katika hatua nyingine, kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika jana (Desemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, kimezingatia upungufu uliopo katika utekelezaji wa matumizi ya tiketi za elektroniki.
    Hivyo, Kamati hiyo imeiagiza Sekretarieti ya TFF kuwasiliana na benki ya CRDB inayoendesha mfumo huo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kuhusu upungufu huo na kuhakikisha unafanyiwa kazi.

    Aidha, Kamati ya Utendaji ya TFF imerejea mazungumzo kati yake na ujumbe wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) uliokuwa nchini ukiongozwa na Meneja wa Vyama Wanachama wa FIFA, James Johnson.  
    Mazungumzo hayo kuhusu Katiba ya TFF yalifanyika Desemba 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
    Kamati ya Utendaji inasubiri rasimu ya Katiba hiyo kutoka FIFA ili iweze kufanya utaratibu wa kuwaarifu wanachama wake juu ya maudhui ya rasimu hiyo.
    Shughuli ya FIFA kurekebisha katiba za nchi wanachama wake inaendelea duniani kote, na kwa Afrika kazi hiyo imekamilika katika nchi za Namibia, Zimbabwe na Malawi.
    Wakati huo huo: Kamati ya Utendaji imepitia na kupitisha makubaliano ya ushirikiano kati ya TFF na Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA).
    Makubaliano hayo ni ushirikiano katika nyanja za mpira wa miguu wa vijana, maendeleo ya waamuzi, ufundi, menejimenti ya matukio (event management) na utafutaji udhamini (sponsorship).
    Kamati ya Utendaji pia jana ilijadili rasimu ya Kanuni za Leseni za Klabu (Club Licensing Regulations), na kuagiza Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ifanye marekebisho ya mwisho, kabla ya kanuni hizo kusainiwa na kuanza kutumika.
    Kamati hiyo chini ya Rais Jamal Malinzi, imepokea taarifa ya maendeleo ya mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (Football Development Fund- FDF).
    Imeipongeza Kamati ya Mfuko huo inayoongozwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodegar Tenga, na kuitaka fanye jitihada za kukamilisha rasimu ya kanuni za uendeshaji mfuko huo.
    Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wa mfuko huo ni Ayoub Chamshama, Ephraim Mafuru, Frederick Mwakalebela, Tarimba Abbas na Zarina Madabida. Sekretarieti ya mfuko huo inaundwa na Henry Tandau ambaye ni Katibu, Wakili Emmanuel Muga na Boniface Wambura.
    FDF ambao ni mfuko utakaokuwa unajitegemea utakuwa unashughulika na maendeleo ya mpira wa miguu kwa vijana, na nyanja nyingine za maendeleo kwa mchezo huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUTANO MKUU TFF MACHI 14 SINGIDA, MATUMIZI YA TIKETI ZA ELEKTRONIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top