• HABARI MPYA

    Wednesday, December 17, 2014

    SIMBA SC YASHINDA KESI YA ETOILE, FIFA YAAMURU WALIPWE MILIONI 500 MAUZO YA OKWI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeshinda kesi dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia kuhusu mshambuliaji Emmanuel Okwi na italipwa dola za Kimarekani 300,000 pamoja na fidia.
    Simba SC iliishitaki Etoile Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kwa kushindwa kulipa fedha za kumnunua Okwi Januari mwaka jana, dola 300,000, zaidi ya Sh. Milioni 500 za Tanzania.
    Etoile iligoma kulipa ikidai inakabiliwa na hali mbaya kifedha, lakini ilionekana kama ni visa baada ya kutofautiana na mshambuliaji huyo wa Uganda.
    Okwi alitibuana na Etoile na kuondoka baada ya miezi sita tangu ajiunge nayo. Klabu ilidai mchezaji alichelewa kuripoti baada ya kupewa ruhusa ya kujiunga na timu ya taifa na kumkata mshahara.
    Emmanuel Okwi kushoto akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe wakati anarejea nyumbani Agosti mwaka huu

    Okwi hakuridhika kukatwa mshahara akafungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na wakati sakata lao likiendelea, akaomba apewe ruhusa ya kucheza klabu nyingine kunusuru kipaji chake.
    Mshambuliaji huyo akapewa ruhusa ya kuchezea klabu yake ya zamani, SC Villa ya kwao, Uganda ambayo nayo kufika Desemba mwaka jana ikamuuza Yanga SC.
    Okwi tena akatofautiana na Yanga SC iliyomsajili kwa Mkataba wa miaka miwii na Nusu na kurejea Simba SC Agosti mwaka huu.
    Ilibidi kesi yake iamuliwe na TFF baada ya Yanga SC, kwanza kumuandikia barua ya kuvunja naye Mkataba na baadaye aliposaini Simba SC ikakana haijamuacha.
    Lakini Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ilipopitia kesi hiyo ikagundua Yanga SC ilivunja Mkataba na Okwi , hivyo akapewa ruhusa ya kuendelea na kazi Simba SC.
    Awali, Okwi alisaini Mkataba wa miezi sita Simba SC kabla ya jana kuongeza miaka miwili.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YASHINDA KESI YA ETOILE, FIFA YAAMURU WALIPWE MILIONI 500 MAUZO YA OKWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top