• HABARI MPYA

    Friday, January 30, 2015

    SAMATTA AREJEA LUBUMBASHI, ATETA NA BOSI WA AZAM FC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta amerejea jana mjini Lubumbashi kuendelea na maisha chini ya utawala wa Moise Katumbi Chapwe, rais wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Samatta akiwa na Mtanzania mwenzake anayecheza naye Mazembe, Thomas Ulimwengu wamepiga picha na mmoja wa Wakurugenzi wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam iliyo ziarani Lubumbashi, Jamal Bakhresa.
    Na jamal Bakhresa ameituma picha hiyo BIN ZUBEIRY jana akisema amefurahi kukutana na vijana na kuzungumza nao mawili matatu. 
    Mbwana Samatta kulia akiwa na Jamal Bakhresa na Thomas Ulimwengu kushoto jana mjini Lubumbashi

    Habari zaidi kutoka Lubumbashi zinasema kwamba, klabu ya CSKA Moscow ya Urusi iliamua kuachana na Samatta kwa sasa baada ya kuumia enka akiwa katika wiki ya kwanza ya majaribio.
    Kiongozi mmoja wa Mazembe ambaye hakupenda kutajwa jina, ameiambia BIN ZUBEIRY jana usiku kwamba timu hiyo ya Ulaya ilivutiwa na uwezo wa mshambuliaji huyo wa Tanzania, lakini ilishindwa kumtathmini zaidi baada ya kuumia.
    Hata hivyo, amesema klabu (TP Mazembe) chini ya Rais, Moise Katumbi bado wapo bega kwa bega kuhakikisha wanatimiza ndoto za mtoto wa Mbagala, Samatta kucheza Ulaya kwa maslahi makubwa.
    Mapema mwezi huu, Samatta alipata fursa ya kufanya mazoezi na klabu ya CSKA Moscow ya Urusi ambayo ilikuwa inamjaribu kwa ajili ya kumnunua, hata hivyo bahati mbaya kwake aliumia enka.
    Samatta ambaye amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake TP Mazembe tangu asajiliwe kutoka Simba SC ya Dar es Salaam, alipania mno Januari hii kuhamia Ulaya, lakini inaonekana wakati wake bado. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AREJEA LUBUMBASHI, ATETA NA BOSI WA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top