• HABARI MPYA

    Wednesday, February 11, 2015

    BEKI LA SIMBA’ LAAHIDI KUWAKILISHA TANZANIA, KENYA

    Na Vincent Malouda, NAIROBI
    ALIYEKUWA beki wa Simba SC David Naftali Tevelu ameahidi kuwakilisha taifa lake vyema katika ligi kuu ya taifa la Kenya akivalia jezi ya Ushuru FC pindi tu msimu wa 2015 utakapong’oa nanga mwishoni mwa mwezi Februari.
    Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY, Tevelu alithibitisha uhamisho wake kutoka Bandari FC ya Mkoa wa Pwani hadi Ushuru FC ya Mkoa wa Nairobi kwa mwaka mmoja.
    “Nimejiunga na Ushuru FC kwa mkataba wa mwaka mmoja kutoka Bandari nilikokuwa kwa miaka minne sasa,” alisema.
    “Naamini mazingira haya mapya yatanisaidia katika mchezo wangu. Kwa sasa natia bidii mazoezini ili niweze kuwafurahisha walimu maana hii ni timu mpya na mchezaji yeyote mgeni lazima atie bidii ndiposa kuonyesha uwezo wake uwanjani,”
    David Naftali (mbele) katika Ligi ya Kenya

    “Nipo tayari kwa msimu huu, mwalimu wangu Ken Kenyatta akinipa nafasi bila shaka nitamfrahisha na timu iweze kusajili matokeo mazuri. Kwa watanzania wenzangu kule nyumbani, nipo hapa (Kenya), kwa ajili yao na katu sitoshusha hadhi ya taifa letu katika ligii kuu ya Kenya. Nitajituma kwa uwezo wangu niwafurahishe hata walimu wa Taifa Stars.”
    Tevelu ni mchezaji pekee mwenye uraia wa Tanzania katika ligii kuu ya Kenya kwa sasa. Kabla ya kujiunga na Bandari mwaka 2011, beki huyo alikuwa akiwajibikia Wekundu wa Msimbazi alikokuwa tangu mwaka 2007.
    Mzawa huyo wa Mbeya aliwahi pia kuichezea AFC Arusha mwaka 2006. Anakuwa mchezaji wa kumi na tano kujiunga na klabu hiyo inayofadhiliwa na Kampuni ya kutoza Ushuru, Kenya (KRA).
    Ivo Phillip Mapunda (Bandari na Gor Mahia), Idris Rajab na Salim Kinje (AFC Leopards) ni baadhi ya Watanzania waliokuwa wakisaka pato lao Kenya vilabuni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BEKI LA SIMBA’ LAAHIDI KUWAKILISHA TANZANIA, KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top