• HABARI MPYA

    Tuesday, February 10, 2015

    YULE BEKI ALIYEMKABA TAMBWE ADAI MAGAZETI ‘YALIBUMBA’ PICHA

    Na Baraka Kizuguto, DAR ES SALAAM
    BEKI wa Ruvu Shooting ya Pwani, George Michael Osei ameyatuhumu magazeti kutengeneza picha inayomuonyesha akimkaba mshambuliaji wa Yanga SC, Amisi Tambwe- lakini utetezi huo haujamsaidia kuepuka adhabu.
    Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu beki huyo kutokana na makosa ya kinidhamu aliyoyafanya akiwa uwanjani.
    Osei ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumkaba na kumchezea kibabe mshambuliaji wa Yanga, Amisi Tambwe ambapo ni kinyume na mchezo wa kiungwana (fair play) ameadhibiwa kwa kuzingatia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
    George Michael kulia amedai magazeti yalitengeneza picha anamkaba Tambwe ili kumchongea

    Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema Osei alipopewa nafasi ya kujitetea alikana kufanya kosa hilo na kudai magazeti yametengeneza picha hizo. TFF iliwasilisha ushahidi wa magazeti mawili ya Championi na moja la The Guardian kwa kuzingatia  Ibara ya 96(3) ya Kanuni ya Nidhamu ya TFF Toleo la 2012.
    Katika uamuzi wake, Kamati imesema kitendo cha Osei ni kinyume na kanuni ya mchezo wa kiungwana (fair play), na kuongeza kuwa kanuni za TFF kwa makosa kama hayo ni dhaifu, hivyo kuagiza zirekebishwe ili ziweze kuwa kali zaidi.
    Katika hatua nyingine Kamati hiyo, imetupa malalamiko yaliyowasilishwa na TFF dhidi Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona, na Katibu wa Simiyu (SIFA), Emmanuel Sorogo.
    Kwa upande wa Sorogo, Kamati imesema baada ya kupitia vielelezo vya pande zote, hasa upande mlalamikiwa imeridhika kuwa hakushiriki katika kumpiga refa kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake kati ya Shinyanga na Simiyu.
    Badala yake aliyehusika ni Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye tayari uongozi umeshachukua hatua dhidi yake kwa kumsimamisha kwanza wakati akisubiri kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya SIFA.
    Barua ya kumsimamisha kocha huyo ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa TFF na Mkurugenzi wa Mashindano. Kamati imeyachukulia maneno ya mlalamikiwa kuwa ni sahihi ndiyo maana hayakupingwa na TFF, hivyo malalamiko dhidi ya mlalamikiwa hayana msingi na yametupwa.
    Kwa upande wa Galibona ambaye ripoti za Kamishna na refa zilionyesha kuwa alishiriki kuhamasisha marefa kupigwa baada ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Polisi Mara FC na Mwadui FC, Kamati imesema mlalamikiwa aliwasilisha vielelezo vinne kuthibitisha kuwa hakuhusika.
    Kamati imesema licha ya ripoti ya Saleh Mang'ola kumtaja Galibona, lakini maelezo ya refa huyo na msaidizi wake Rebecca Mulokozi waliyoandika Kituo cha Polisi baada ya tukio hilo hayakumtaja mlalamikiwa mahali popote.
    Barua ya FAM pia kwenda TFF kuhusu matukio ya mechi hiyo yanamtoa hatiani mlalamikiwa, hivyo Kamati imeamuru kuwa malalamiko dhidi ya Galibona hayana msingi na yametupiliwa mbali.
    Aidha, Kamati ya TFF imempiga faini ya sh. 600,000 au kifungo cha mwaka mmoja Katibu Mkuu wa Villa Squad, Mbarouk Kassanda kwa kusika na uhamisho wa mchezaji Omari Ramadhan ambao haukufuata kanuni za usajili.
    Villa Squad iliingiza majina tofauti ya mchezaji huyo wa African Lyon, ambapo badala ya Omari Ramadhan ikaingiza Omari Issa Ibrahim'. Kamati imeona Villa Squad ilifanya hivyo ili kudanganya, kuwezesha mfumo wa usajili wa kielektroniki ukubali jina la mchezaji.
    Malalamiko ya kutaka kupewa pointi tatu na mabao matatu kwenye mechi dhidi ya Villa Squad kwa kumchezesha mchezaji huyo, yametupwa na Kamati kwa sababu alikuwa ni mchezaji halali aliyethibitishwa (eligible) na TFF.
    Kamati ilimuita mchezaji huyo na kumhoji kama alishiriki au alifahamu udanganyifu wa kubadili majina ili aweze kuingizwa katika mfumo wa eletroniki wa usajili lilibaki kuwa suala la mashaka. Inawezakana alishiriki au hakushiriki; Kamati haikupata ushahidi thabiti. Hivyo, Kamati iliamua kumpa mchezaji faida ya mashaka (benefit of doubts) na hivyo kutompa adhabu yoyote.
    Kassanda ameadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 40(11) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) wakati Omari Ramadhan ni mchezaji wa African Lyon kwa vile ana mkataba na klabu hiyo.
    Katika hatua nyingine, JKT Mlale imeamriwa kuilipa African Lyon jumla ya sh. 600,000 ikiwa ni ada ya uhamisho na fidia kwa kumtumia mchezaji Noel Lucas kinyume cha taratibu kwenye mechi.
    Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji baada ya kusikiliza malalamiko ya African Lyon ambapo ilibaini kuwa klabu hiyo ilikubali kulipwa sh. 300,000 ilikwa ni ada ya uhamisho.
    Kamati imekataa maombi ya African Lyon kutaka pointi tatu na mabao matatu katika mechi yao ambapo Noel Lucas alicheza, kwa vile mchezaji huyo usajili huo ulithibitishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Pia JKT Mlale imetakiwa kuilipa African Lyon sh. 300,000 nyingine za usumbufu wa kufuatilia malipo ya mchezaji huyo. JKT Mlale imetakiwa kulipa fedha hizo kabla ya mechi yake ya mwisho ya ligi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YULE BEKI ALIYEMKABA TAMBWE ADAI MAGAZETI ‘YALIBUMBA’ PICHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top