• HABARI MPYA

    Monday, March 30, 2015

    MALINZI: SAMATTA, ULIMWENGU NA MWINYI MFANO WA KUIGWA

    Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi amesema wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars wanaocheza nje ni mfano wa kuigwa kwa wenzao wanaocheza hapa.
    Stars jana ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Malawi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jana kikosini ikiwa na vijana watatu wanaocheza nje, kiungo wa Al Markhiya ya Qatar, Mwinyi Kazimoto Mwitula na washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samaatta na Thomas Ulimwengu.
    Na kuhusu vijana hao, Malinzi amesema; “Vijana wanaocheza nje, wameonyesha matunda ya mafunzo wanayopata huko, kwa maana ya mbinu, ufundi, utimamu wa mwili na uimara. Ni mfano wa kuigwa,”amesema.
    Rais Malinzi kushoto jana Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza

    Pamoja na hayo, Malinzi ameipongeza timu kwa ujumla jana akisema kwamba walikutana na mechi ngumu, lakini wakajitahidi kupata sare.
    “Naipongeza Taifa Stars kwa kiwango cha leo. Mechi ilikuwa ngumu, matokeo haya bila shaka kwa viwango vya FIFA yataipandisha timu mwezi ujao, maana Malawi wako juu yetu,”amesema Malinzi.
    Aidha, Rais huyo wa TFF amesema maboresho ya timu yanaendelea na mwezi ujao, kikosi cha pili cha timu ya taifa, maarufu kama Taifa Stars Maboresho kitacheza mechi ya kujipima nguvu kabla ya kupata kikosi cha mwisho kitakachokwenda Afrika Kusini kushiriki michuano ya COSAFA.
    Katika mchezo wa jana, Stars iliponea chupuchupu kufungwa kama si Mbwana Ally Samatta kusawazisha bao dakika ya 76 akiwa katikati ya mabeki wawili wa The Flames, baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa.   
    Esau Kanyenda alianza kuifungia Malawi dakika ya tatu tu ya mchezo, baada ya kuuwahi mpira uliorudi kufuatia kona ya Haray Nyirenda kuzua kizaa langoni mwa Taifa Stars.
    Stars ilishindwa kuupasua ukuta wa The Flames kipindi cha kwanza na nafasi pekee nzuri ilikuwa dakika ya 14, lakini shuti la Samatta likaokolewa na kipa McDonald Marava.
    Zaidi ya hapo, Amri Kiemba alipiga nje dakika ya 17 akiwa kwenye nafasi nzuri na Shomary Kapombe akapiga juu ya lango dakika ya 19 baada ya krosi nzuri ya Haroun Chanongo.
    Kipindi cha pili, Stars ilibadilika baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Mart Nooij akiwatoa viungo Amri Kiemba na Chanongo na kuwaingiza Ngassa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
    Stars ilipiga ziara kwenye lango la Malawi kwa dakika zote tano za mwisho kusaka bao la ushindi, lakini bahati haikuwa yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI: SAMATTA, ULIMWENGU NA MWINYI MFANO WA KUIGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top