• HABARI MPYA

    Monday, March 30, 2015

    NGASSA AMERUDI KWENYE ‘FOMU’, ASEMA THOM ULIMWENGU

    Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
    MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Thomas Emmanuel Ulimwengu amefurahishwa na kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa kurejea katika kiwango chake.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Ulimwengu alisema kwamba sasa anamuona Ngassa halisi uwanjani, akicheza kwa kiwango cha juu tofauti na siku za katikati.
    “Ngassa alikuwa hayupo kabisa mchezoni katikati hapa, kwa kweli ilikuwa inanisikitisha sana. Lakini kwa sasa amerudi, amenifurahisha sana na ninaomba aendelee hivyo hivyo,”amesema Ulimwengu.
    “Nasikia amepata timu nje, itakuwa vizuri akiondoka hapa. Nisingependa kuona mpira wake unaishia hapa. Namtakia kila la heri, Ngassa ni mchezaji mzuri na umri bado unamruhusu. Popote anaweza kufanya vizuri,”amesema Ulimwengu.
    Mrisho Ngassa (katikati) alitokea benchi jana kwenda kuseti bao la kusawazisha la Stars
    Thomas Ulimwengu kulia amesema Ngassa amerudi kwenye 'fomu'

    Ngassa alitokea benchi jana na kwenda kutengeneza bao la kusawazisha, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikitoa sare ya 1-1 na Malawi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Ngassa baada ya kwenda kumpokea Haroun Chanongo, alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Malawi, kabla ya kwenda kuwapiga chenga mabeki watatu hadi ndani ya boksi, akampasia mshambuliaji mwingine wa TP Mazembe, Mbwana Samatta kufunga bao dakika ya 76.
    Kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, Ngassa alikuwa akicheza chini ya kiwango na zaidi ilielezwa ilitokana na kuvurugwa na klabu yake, Yanga SC kutokana na mkopo wa benki Sh. Milioni 45.
    Ngassa alisaini Yanga SC mwaka juzi akitokea kwa mahasimu Simba SC, alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Azam FC, lakini baadaye akaambiwa alikuwa ana mikataba na klabu zote hizo mbili.
    Simba SC walidai baada ya Ngassa kumaliza Mkataba wake wa mkopo kutoka Azam FC, walimuongezea Mkataba na wakampa Sh. Milioni 35.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaamuru Ngassa arejeshe fedha za Simba SC na faini ya Sh. Milioni 10 juu pamoja na kumfungia mechi sita za Ligi Kuu msimu uliopita.      
    Yanga SC wakamchukulia mkopo benki na kulipa fedha za Simba, wakiahidi kumsaidia kumlipa mkopo huo.
    Hata hivyo, baadaye Ngassa akawa analalamika anakatwa zaidi na wakati mwingine hapati kabisa mishahara- huku deni likiwa halipungui na zaidi akalalamika Yanga hawamsikilizi.
    Hata hivyo, kufuatia habari za mchezaji huyo kupata timu nje, Ngassa ameonekana mwenye furaha tena na kucheza kwa kiwango kile ambacho kilimjengea heshima katika soka ya Tanzania.
    Ngassa mwenyewe bado hajathibitisha kuhusu kuondoka Yanga SC, ingawa Mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu- bali magazeti yamekuwa yakiandika mara anakwenda Afrika Kusini, mara Qatar.
    BIN ZUBEIRY inafahamu klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini ilijaribu bila mafanikio kumnunua Ngassa kutoka Yanga SC mwaka jana, baada ya kushindwa kuafikiana dau na klabu yake ya sasa.
    El Merreikh ya Sudan ilijaribu kumnunua Ngassa bila mafanikio Desemba mwaka 2012, kufuatia mchezaji mwenyewe kugoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA AMERUDI KWENYE ‘FOMU’, ASEMA THOM ULIMWENGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top