• HABARI MPYA

    Friday, April 17, 2015

    ETOILE WATUA DAR NA MKWARA WA KUIPIGA YANGA TATU, KOCHA WAO ‘AGEUKA BUBU’ KISA UCHOVU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WAPINZANI wa Yanga katika Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, Etoile Sportive du Sahel (ESS) ya Tunisia wamewasili Dar es Salaam Alfajiri ya leo na kutamba kuwafunga wenyeji mabao matatu.
    Kocha Mkuu wa timu hiyo, Faouzi Benzarti aligoma kuzungumza akidai hajui Kiingereza na pia amechoka baada ya safari ya saa tisa angani kutoka Tunisia, kupitia Sudan, ambako waliwateremsha ndugu zao, Esperance wanaocheza na El Merreikh kesho.
    Lakini mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Moussa Sofien ametamba watashinda mabao matatu Uwanja wa Taifa kesho.
    Benzarti ambaye amefundisha karibu timu zote kubwa Tunisia na nyingine za Uarabuni na Kaskazini mwa Afrika, ikiwemo Raja Cassablanca ya Morocco, alielekea moja kwa moja kwenye gari na kusema; “Siwezi kuzungumza chochote, nimechoka, safari ndefu saa tisa,”.
    Lakini Sofien akiwa kwenye gari alifungua kioo na kuwaonyesa Waandishi wa Habari vidole vitatu, akimaanisha watawafunga wapinzani wao, Yanga mabao matatu. 
    Moussa Sofian akionyesha vidole vitatu akiwa kwenye basi lililowapokea JNIA Alfajiri ya leo
    Wachezaji wa Etoile kwenye basi lao tayari kwa safari ya hotelini
    Wanapanda basi kuelekea Kunduchi
    Wanatoka ndani ya Uwanja wa Ndege wa JNIA
    Kocha Faouzi Benzarti alikataa kuzungumza kwa sababu ya uchovu wa safari

    Etoile du Sahel wametua Saa 10:10 Alfajiri kwa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56 kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Msafara wao umeongozwa na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia (FTF), Krifa Jalel na wamekuja pia na Rais wa klabu yao, Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, Waandishi wa Habari 12 na wapenzi 10.
    Baada ya kutoka ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Etoile du Sahel waliopokewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro, walielekea katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi.
    Jioni ya leo, mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa mwaka 2007 na washindi wa pili wa 2004 na 2005 wanatarajiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambako mechi itachezwa kesho.
    Kwa ujumla wachezaji wa Etoile, mabingwa wa Kombe la Shirikisho mwaka 2006, lililokuwa Kombe la Washindi 1997 na 2003, lililokuwa Kombe la CAF 1995 na 1999 na Super Cup 1998 na 2008, walionekana wako vizuri licha ya kulalamikia uchovu.
    Wachezaji wa timu hiyo walipoingia kwenye basi lao walianza kuimba na kupiga makofi kuashiria wana morali nzuri kuelekea mchezo huo.
    Marefa wa mchezo huo, Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na Kamisaa Salah Ahmed Mohamed kutoka wote waliwasili mapema jana na kufikia hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.
    Wakati ESS iliyoanzia Raundi ya Kwanza ambako iliitoa Benfica ya Luanda kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 1-0 kwao na kulazimisha sare ya 1-1 Angola, Yanga ilizitoa BDF ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2 katika Raundi ya Awali na FC Platinum ya Zimbabwe kwa jumla ya mabao 5-2 katika Raundi ya Kwanza.
    Yanga SC tangu imalize mchezo wake wa Ligi Kuu na Mbeya City Jumamosi ambao ilishinda 3-1, imekuwa kambini katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, ikifanya mazoezi Uwanja wa Karume na Taifa kujiandaa na mechi hiyo ya kesho. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ETOILE WATUA DAR NA MKWARA WA KUIPIGA YANGA TATU, KOCHA WAO ‘AGEUKA BUBU’ KISA UCHOVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top